DAR ES SALAAM: MASHINDANO ya soka kati ya Kenya na Tanzania yanatarajiwa kuchukua mkondo mpya mwezi ujao huku mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga SC wakiwakaribisha Bandari FC ya Kenya katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa klabu unaotarajiwa kuchezwa Septemba 12 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mechi hiyo itakuwa kilele cha Siku ya Mwananchi ambayo inaambatana na Tamasha la kila mwaka la mashabiki wa Yanga linaloadhimisha utambulisho wa klabu na kuunganisha mashabiki na wachezaji kabla ya msimu mpya.
Licha ya kutajwa kuwa ni mechi ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya, mchezo huo unavuta hisia za wengi kutokana na mvutano wa hivi karibuni wakati wa michezo ya CHAN inayoendelea, ambapo timu za taifa za Tanzania (Taifa Stars) na Kenya (Harambee Stars) ziliingia katika uhasama wa kishabiki.
Yanga ilikuwa na wachezaji wanne kwenye kikosi cha Taifa Stars, wakiongozwa na fowadi Clement Mzize.
Tayari mvutano unaongezeka kabla ya pambano hilo, huku msemaji wa Yanga, Ali Kamwe akieleza kuwa mechi hiyo ina umuhimu mkubwa kitaifa zaidi ya soka la klabu.
“Hii haitakuwa mechi ya kirafiki tu. Nataka Wakenya wasikie hili tumekabidhi matatizo yetu ya kitaifa kwa Yanga. Watatetea Tanzania dhidi ya Kenya,” Kamwe alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bandari FC, Tony Kibwana, timu hiyo itasafiri hadi Tanzania Agosti 30 kwa kambi ya maandalizi ya msimu mpya itakayojumuisha mfululizo wa mechi dhidi ya wapinzani wao hao.
“Tutaondoka Mombasa Agosti 30 kuelekea Tanzania, ambapo tutakuwa na maandalizi ya msimu mpya, ikijumuisha mashindano na vilabu mbalimbali vya ndani. Kilele kitakuwa dhidi ya Yanga FC wakati wa Mwananchi Day,” Kibwana alithibitisha.
Kibwana aliongeza kuwa wakati timu hiyo ikiwa imepoteza wachezaji wachache muhimu, wamejipanga kuzindua wachezaji wapya ambao anaamini watakuwa na matokeo makubwa.
“Ndiyo, tumepoteza wachezaji muhimu, lakini hivi karibuni tutatambulisha safu yetu mpya, na nina imani watafanya maajabu,” alisema.
Bandari ilichangia wachezaji watano kwenye kikosi cha Harambee Stars CHAN, akiwemo kipa Farouk Shikalo, ambaye anarejea katika eneo alilozoea, baada ya kucheza ligi ya Tanzania.
The post Mwananchi Day; Yanga kukipiga na Bandari ya Kenya first appeared on SpotiLEO.