DAR ES SALAAM: TIMU ya mpira wa kikapu ya JKT inatarajia kuzindua rasmi wa uwanja wao wa kikapu wa JKT Mgulani, uliokarabatiwa kwa ushirikiano na kampuni ya michezo ya kubahatisha.
Kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo leo, uzinduzi huo utafanyika kesho kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi, katika viwanja vya JKT Mgulani, Dar es Salaam.
Taarifa hiyo imewahimiza viongozi wa michezo, wadau wa kikapu, wachezaji wa zamani, na wapenzi wote wa mchezo huo, kuhudhuria tukio hilo muhimu kwa maendeleo ya mpira wa kikapu nchini.
“Tunayo furaha kuwakaribisha kwenye uzinduzi huu wa kihistoria. Uwanja huu umekarabatiwa kwa viwango bora kabisa na sasa uko tayari kutumika kwa mechi na mazoezi ya kiwango cha juu.
“Tunapenda kuwashukuru Premier Bet kwa kushirikiana nasi kufanikisha jambo hili,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Katika kusherehekea tukio hilo, kutakuwa na mchezo wa ufunguzi kati ya JKT na Dodoma Spurs, timu mbili zenye historia na ushindani mkubwa katika ligi ya mpira wa kikapu nchini.
“Hii ni siku ya heshima kwa kikapu cha Tanzania. Tunakaribisha kila mmoja ajitokeze kwa wingi kushuhudia tukio hili la kihistoria,” imeeleza taarifa hiyo.
The post JKT Kikapu kuzindua uwanja wake kesho first appeared on SpotiLEO.