MADRID: KIUNGO wa Manchester City anayeshikilia tuzo ya Ballon d’Or Rodrigo Cascante Hernandez maarufu ‘Rodri’ na mkongwe wa Real Madrid Dani Carvajal wameitwa kwenye timu ya taifa Hispania kwa mechi zijazo za kufuzu kwa Kombe la Dunia baada ya kukosekana kwa muda mrefu kwa sababu ya majeraha ya goti.
Kocha wa Hispania Luis de la Fuente aliwajumuisha vinara hao katika kikosi chake kilichotangazwa leo Ijumaa kwa michezo dhidi Bulgaria na Uturuki Septemba 4 na 7, huku bingwa huyo wa Ulaya akisaka nafasi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026.
Rodri alikaa nje karibu msimu mzima uliopita baada ya kuupata jeraha la ACL katika goti lake la kulia mwaka mmoja uliopita. Kisha akaripotiwa kupata tena jeraha kwenye paja lake, katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu.
Kocha wa Manchester City Pep Guaridola sasa anampa muda wa mechi ili kuzoea uwanja na alikosa mechi ya kwanza ya Ligi Kuu, kwenye ushindi wa 4-0 dhidi ya Wolves, na akaingia kama mchezaji wa akiba katika mchezo walioupoteza kwa mabao 2-0 mbele ya Tottenham wikendi iliyopita.
Carvajal alipata jeraha la ACL katika goti lake la kulia Oktoba mwaka jana. Alirejea Madrid mwezi Julai na alianza kwa mara ya kwanza tangu aliporejea wikendi iliyopita katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Real Oviedo kwenye ligi ya Hispania.
De la Fuente pia amemuita kwa mara ya kwanza kinda wa Como ya Italia Jesús Rodríguez. Winga huyo mwenye umri wa miaka 19 alijiunga na timu ya Cesc Fabregas msimu huu kutoka Real Betis.
The post Rodri, Carvajal waitwa Hispania first appeared on SpotiLEO.