ZANZIBAR – KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Morocco, ameweka wazi kuwa kikosi chake kipo tayari kwa vita ya pointi tatu kesho dhidi ya Niger katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Pamoja na maandalizi mazuri, amesema bado wana changamoto katika eneo la namba tisa.
“Tumekuja Zanzibar tukiwa na morali kubwa, wachezaji wako salama na mazoezi tumeyakamilisha kwa mafanikio.
“Nimeona ari kubwa na kujituma kwa vijana. Hata hivyo, bado tuna changamoto katika eneo la namba tisa ambalo tunalifanyia kazi, kwa sababu tunahitaji mshambuliaji anayeweza kumaliza nafasi tunazozipata,” alisema Morocco wakati akizungumza na waandishi wa habari leo.
Ameongeza kuwa mchezo huo ni nafasi ya kuonesha mwelekeo mpya wa Stars na kutoa faraja kwa Watanzania wanaoamini katika kikosi hicho.
Kwa upande wake, mchezaji wa kikosi hicho, Simon Msuva, ametuma ujumbe wa kuwatia moyo mashabiki akisema wachezaji wamejipanga kupambana hadi mwisho.
“Tunajua mchezo wa kesho si rahisi, lakini kila mmoja wetu yupo tayari kwa ajili ya taifa. Umoja ndani ya timu ni mkubwa na tunahitaji Watanzania waendelee kutuunga mkono. Tutapigana kwa ajili ya bendera ya nchi,” alisema Msuva.
Stars na Niger wamekutana mara tatu kwenye michezo ya kimashindano na kirafiki, huku kila upande ukishinda mara moja na mechi moja ikimalizika kwa sare. Matokeo hayo yanaweka mizani sawa, jambo linaloongeza ladha ya mchezo wa kesho.
Taifa Stars ipo katika kundi E la kufuzu Kombe la Dunia 2026 likiwa na Morocco, Zambia, Niger na Congo, baada ya Eritrea kujiondoa. Morocco tayari imefuzu ikiwa kinara kwa alama 18, huku Stars wakishika nafasi ya pili kwa pointi 10. Zambia na Niger wanashikilia alama 6 kila moja, wakati Congo ikiburuza mkia kwa pointi moja pekee.
The post Stars iko tayari kuivaa Niger kesho first appeared on SpotiLEO.