DODOMA: SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesitisha rasmi mchakato wa uchaguzi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) uliokuwa umepangwa kufanyika Oktoba 4, 2025.
Uamuzi huo umetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Professa Palamagamba Kabudi baada ya kubaini kuwa uongozi wa TOC ulitangaza uchaguzi kwa kutumia katiba isiyo halali.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa Dar es Salaam Leo na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini, Hassan Mabuye, Katiba inayotambuliwa kisheria na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ni ile iliyoidhinishwa Novemba 26, 2020.
Akitoa ufafanuzi, Mabuye, alisema Wizara imechukua hatua hiyo kwa kuzingatia misingi ya demokrasia, uwajibikaji, utawala bora na utulivu katika sekta ya michezo.
Miongoni mwa maelekezo yaliyotolewa na Waziri ni: Kusimamishwa mara moja kwa mchakato wa uchaguzi uliotangazwa na TOC.
Kuanzishwa mara moja kwa mchakato mpya wa uchaguzi wa TOC kwa mujibu wa Katiba sahihi na taratibu zote zinazotambuliwa na Serikali.
Aidha, Wizara imesisitiza kuwa rufaa iliyowasilishwa na uongozi wa TOC kuhusu zuio la awali la Msajili wa Vyama vya Michezo, ilikataliwa, na hivyo ni lazima kufuata maelekezo ya Serikali.
Mabuye aliongeza kuwa wadau wote wa michezo nchini wanaelekezwa kushirikiana katika mchakato mpya utakaozingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali ili kulinda maslahi mapana ya michezo ndani na nje ya nchi.
The post Serikali yasitisha uchaguzi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania first appeared on SpotiLEO.