DAR ES SALAAM: MAKOCHA wa Simba na Yanga Fadlu Davids na Romain Folz Kila mmoja amekiri kikosi chake kiko vizuri kupambania ushindi katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam Leo, Fadlu amesema wachezaji wake wana morali ya mechi kubwa na wapo tayari kwa ajili ya kwenda kwenye mechi ya kesho kuhakikisha wanapambana na kupata ushindi.
“Tuko tayari kupambana kupata ushindi ambao utakuwa muhimu kwetu kwa kuanza msimu na taji la kwanza,”amesema Fadlu.
Kwa upande wake, Kocha Folz amesema wana shauku kubwa ya matokeo mazuri, wanakwenda kucheza mchezo mkubwa, lazima wahakikishe mashabiki wanapata kile ambacho wanahitaji.
“Tunakwenda kwenye mchezo mkubwa, tunapaswa kuwaheshimu wapinzani na tumejiandaa kukabiliana na kila hali ya mchezo”-Romain Folz
Amesema ana kundi kubwa la wachezaji wazuri ambao wanaweza kumudu mazingira ya mchezo wowote, wamejiandaa vizuri kimwili na kiakili.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi wa kati Ahmed Arajiga, waamuzi wasaidizi ni Mohamed Mkono, Kassim Mpanga na wa akiba ni Ramadhan Kayoko.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetaja viingilio kuwa ni sh 300,000 kwa viti vya platnum,VIP sh 100,000,VIP B sh 30,000, C sh 20,000, viti vya orange sh15,000 na mzunguko sh 5000.
The post Simba, Yanga wako tayari kwa Ngao ya Jamii kesho first appeared on SpotiLEO.