GABORONE: KOCHA Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davids amesema wanawaheshimu wapinzania wao hivyo, watashuka dimbani kwa tahadhari kutimiza malengo yao ya kuondoka na ushindi.
Amesema kikosi chake kimejipanga kuhakikisha kinashinda michezo yote ya nyumbani na ugenini ili kufanikisha safari ya kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza Leo kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Gaborone United ya Botswana, Davids alibainisha kuwa maandalizi ya kikosi chake yamekuwa bora kutokana na mechi mbili ngumu walizocheza hivi karibuni, ikiwemo Simba Day na Ngao ya Jamii.
“Kwenda hatua ya makundi unahitaji kushinda mechi zote nyumbani na ugenini na sisi tumejiandaa kufanya hivyo. Timu yangu imecheza mechi mbili zenye uzito mkubwa na zimeongeza ubora wetu,” alisema Davids.
Hata hivyo, aliongeza kuwa licha ya maandalizi mazuri, anaiheshimu Gaborone United kwa kuwa wapinzani wanaojua kupambana. “Tunawaheshimu sana wapinzani wetu lakini tunalenga kupata matokeo chanya kuanzia kesho,” alisisitiza kocha huyo.
Simba itacheza mchezo huo ugenini na baadaye kurudiana Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam bila mashabiki, kufuatia adhabu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya tukio la uvamizi wa mashabiki na matumizi ya fataki kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho msimu uliopita.
The post Fadlu: Hatuwaogopi Gaborone UTD first appeared on SpotiLEO.