NEWCASTLE: MENEJA Eddie Howe wa Newcastle United amesema ni pigo kwa klabu yake kuendelea kumkosa mshambuliaji wao mpya Yoane Wissa ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa takriban wiki nyingine nne baada ya kuumia goti akiwa katika majukumu ya timu ya DR Congo.
Akiwa amesajiliwa kwa pauni milioni 55 baada ya sakata la muda mrefu la usajili Brentford ilipokataa ofa za awali za Newcastle, Wissa aliletwa kuziba pengo la ushambuliaji lililoachwa na kuondoka kwa Alexander Isak aliyetimkia Liverpool.
“Kila mtu alitaka Yoane awe fiti, Hakuna kitu kingine tofauti ambacho ningefanya. Tulifanya kila tulichokifanya kama klabu kujaribu kumtunza Yoane”.
“Lakini ni sawa na mchezaji yeyote wa soka anapokwenda kwenye majukumu ya kimataifa, huwezi kudhibiti dakika anazocheza na, kwa bahati mbaya, anaumia na sasa inabidi tukabiliane vyema na hali hiyo”.
“Tunafikiri atakuwa nje hadi baada ya kipindi kijacho cha mapumziko ya kimataifa. Ni kama tunamuwahisha awe fiti kwa mchezo dhidi ya Brighton. Tunatumai tunaweza kufanikiwa na bila shaka, atakuwa mchezaji muhimu sana kwetu.” – Howe aliwaambia waandishi wa habari kuelekea mchezo wa Jumapili dhidi ya Bournemouth.
Jeraha la Wissa linaongeza kazi ya ziada kwa mchezaji mwingine wa Newcastle Mshambuliaji wa Ujerumani Nick Woltemade, ambaye alisajiliwa kutoka Stuttgart kwa mkataba wa rekodi ya klabu wenye thamani ya pauni milioni 69.
The post Jeraha la Wissa lamkosesha raha kocha Howe first appeared on SpotiLEO.