Upepo wa mabadiliko umeanza kuvuma ndani ya klabu ya Simba SC, kufuatia sintofahamu ya muda mrefu kuhusu hatima ya kocha wao mkuu, Fadlu Davids. Taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa uongozi umeanza rasmi mchakato wa kusaka kocha mpya, ikiwa ni hatua ya kujiandaa na maisha mapya iwapo Fadlu ataondoka.
Knee and hip pain sufferers should read this!
Joint Guard
by TaboolaSponsored Links
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini amedaiwa kusimamia msimamo wake wa kuondoka, licha ya vikao kadhaa vilivyofanywa na viongozi wa Simba kumshawishi abaki. Vyanzo vya karibu na klabu vinasema kuwa Fadlu amekuwa akionekana kutoridhishwa na baadhi ya mambo ya kiutendaji, ikiwemo masuala ya usajili na mipango ya timu kwa msimu huu. Kwa mujibu wa taarifa hizo, kuna uwezekano mkubwa baada ya mchezo wa leo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United, uongozi wa Simba ukatoa tamko rasmi kwa umma kuhusu mustakabali wa kocha huyo.
Wakati Simba ikiendelea na taharuki hiyo, usiku wa kuamkia leo klabu ya Raja Casablanca kutoka Morocco imetangaza kumtimua kocha wao mkuu baada ya matokeo yasiyoridhisha.
Hatua hiyo imezidisha uvumi kwamba Fadlu Davids ndiye kinara anayetajwa kurithi mikoba ndani ya klabu hiyo yenye historia kubwa barani Afrika. Vyombo vya habari nchini Morocco vimeweka jina la Fadlu kwenye orodha ya makocha wanaopewa nafasi kubwa kuchukua nafasi hiyo, jambo linaloongeza mashaka kuwa kuondoka kwake Simba SC ni suala la muda tu.
Uongozi wa Simba SC haujakaa kimya. Taarifa za ndani zinaeleza kwamba tayari wameanza kuwasiliana na makocha kadhaa wa kimataifa, wakiwemo waliowahi kupata mafanikio makubwa barani Afrika. Lengo ni kuhakikisha kikosi cha Simba kinabaki imara na mashindano ya msimu huu hayawi na madhara makubwa kutokana na mabadiliko ya benchi la ufundi. Simba, ambao ni mabingwa wa kihistoria nchini Tanzania na washiriki wa kudumu wa michuano ya CAF, wanahitaji uthabiti wa kiufundi hasa msimu huu ambao malengo makuu ni kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kulinda heshima ya ndani kupitia Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA.
Mashabiki wa Simba SC kwa sasa wapo njia panda. Baadhi wanamtetea Fadlu kwa hoja kuwa bado hajapata muda wa kutosha kuonesha mbinu zake kikamilifu, huku wengine wakisisitiza kuwa kocha huyo hana tena moyo wa kuendelea na kazi ndani ya klabu na kwamba ni bora Simba kuanza ukurasa mpya haraka. Wachambuzi wa soka pia wameeleza kuwa kama Fadlu ataondoka, Simba italazimika kuchukua tahadhari kubwa katika kumleta mrithi wake. Kocha mpya atapaswa kuanza kazi akiwa na presha kubwa ya kuhakikisha matokeo ya haraka, huku pia akijenga uhusiano wa karibu na kikosi kilichojaa nyota wenye uzoefu na vijana chipukizi.
Kwa sasa macho na masikio ya mashabiki, wadau na wachambuzi yapo kwenye uongozi wa Simba SC. Kinachosubiriwa sasa ni tamko la wazi la klabu baada ya mchezo wa leo, ambalo litabeba hatma ya kocha huyo na mwelekeo mpya wa Simba SC katika safari yao ya ndani na kimataifa.
#Chanzo: Hans Raphael