PARIS: BEKI wa Paris Saint-Germain, Marquinhos, ameingia kwenye orodha ya majeruhi ya muda mrefu ya klabu hiyo, baada ya timu hiyo ya Ufaransa kuthibitisha leo kwamba mchezaji huyo raia wa Brazil atakuwa nje ya uwanja kwa wiki chache kutokana na jeraha la paja la kushoto.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, aliyejiunga na PSG mwaka 2013 na kuichezea klabu hiyo katika zaidi ya mechi 300 za Ligue 1, amepata jeraha siku chache kabla ya mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona itakayopigwa Jumatano ijayo. Mbali na Marquinhos, Joao Neves, Desire Doue na Ousmane Dembele pia wanauguza majeraha.
Marquinhos alipata jeraha mwishoni mwa mchezo ambao PSG walipoteza 1-0 dhidi ya Olympique Marseille Jumatatu iliyopita.
“Aliniambia anahisi maumivu kidogo. Hakuna chochote kikubwa, lakini tunahitaji tu kuwa makini na kuchukua tahadhari. Ni pigo kwetu kwa sababu Marquinhos ni nahodha wetu, lakini lazima tuwe tayari, na nadhani tuko tayari kwa lolote.” – kocha wa PSG Luis Enrique aliwaambia waandishi wa habari.
Kocha huyo pia alisema hana wasiwasi kuhusu jeraha hilo akisema soka ni mchezo unaoacha athari, na majeraha ni jambo la kawaida jambo muhimu ni kujua jinsi ya kujilinda na kudhibiti majeraha hayo. Amesema PSG ina wachezaji wengi kutoka kwenye akademi yao ambao wanaweza kuingia na kucheza vyema.
Mabingwa hao watakuwa wenyeji wa Auxerre katika mechi ya Ligue 1 kesho Jumamosi.
The post Marquinhos Ajiunga na Orodha ya Majeruhi PSG first appeared on SpotiLEO.