Dar es Salaam. Yanga imesonga mbele katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 nyumbani leo Septemba 27, 2025.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga itinge raundi ya pili kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-0, ikichagizwa na ushindi wa mabao 3-0 ambao iliupata katika mechi ya kwanza iliyocheza ugenini huko Angola, wiki iliyopita.
Mabao yaliyoipa ushindi Yanga katika mchezo wa leo, yote yalipatikana katika kipindi cha pili yakipachikwa na Pacome Zouzoua na Aziz Andabwile.
Kipindi cha kwanza, Yanga ilionekana kutocheza vizuri na hivyo kushindwa kutengeneza nafasi nzuri za mabao ambayo yangeweza kuifanya iimalize mechi mapema na hadi filimbi ya mapumziko ilipopulizwa, timu hizo zilienda katika vyumba vya kubadilishia nguo zikiwa sare tasa.
Ubao wa matokeo ulianza kubadilika katika dakika ya 71 kupitia kwa Zouzoua aliyemalizia kwa ustadi pasi ya Andy Boyeli.
Boyeli alinasa pasi ya Pacome nje kidogo ya lango la hatari la Wiliete na kumrudishia tena pasi Zouzoua ambaye alijikuta akitazamana na kipa wa Wiliete na kuujaza mpira kimiani.
Dakika ya 87, Andabwile aliiandikia Yanga bao la pili akimalizia kwa kichwa mpira wa kona uliochongwa na Offen Chikola.
Matokeo hayo yalidumu hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa.
Wakati Yanga ikisonga mbele, mambo hayakuwa mazuri kwa wawakilishi wa Zanzibar, Mlandege ambao licha ya ushindi wa mabao 3-2 nyumbani dhidi ya Ethiopian Insurance, wameaga mashindano hayo.
Ethiopian Insurance wamesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3 wakibebwa na ushindi wa mabao 2-0 walioupata katika mchezo wa kwanza wiki iliyopita huko Ethiopia.