DAR ES SALAAM:KLABU ya Simba chini ya Kocha Mkuu mpya Dimitar Pantev imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya mabingwa wa Sudan, Al Hilal Omdurman, katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa jana.
Mchezo huo wa kujipima nguvu ulikuwa sehemu ya maandalizi ya Simba kuelekea michezo iliyoko mbele yao Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba wanatarajia kukutana na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini Oktoba 19, mwaka huu mchezo wa raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwatoa Gaborone United ya Botswana.
Huenda Kocha Pantev anatumia fursa ya michezo ya kirafiki ikiwemo huo ili kujipanga vizuri na kuwafahamu zaidi wachezaji wake kabla ya kuanza safari ya kuwafuata Nsingizini.
Mchezo dhidi ya Al Hilal unatajwa kuwa kipimo kizuri kwa Simba, ikizingatiwa kuwa wapinzani wao ni miongoni mwa timu zenye historia kubwa na uzoefu katika soka la Afrika.
Wekundu hao wa Msimbazi wamekuwa katika kiwango bora katika michezo miwili iliyopita ya Ligi Kuu wakiongoza msimamo kwa pointi sita.
The post Pantev aing’arisha Simba ikiichapa Al Hilal first appeared on SpotiLEO.