KLABU ya Simba imethibitisha kuwa mchezaji wao, Mohamed Bajaber ambaye tangu asajiliwe kutoka Police ya Kenya hajaonekana uwanjani kutokana na majeraha, ameanza mazoezi kuelekea kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini chini ya Dimitar Nikolaev Pantev, huku ikitoa ufafanuzi utofauti na Kocha Mkuu na Meneja Mkuu.
Meneja habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema kuwa mchezaji hiyo raia wa Kenya, alisajiliwa akiwa na majeraha kitu ambacho kilimfanya asiweze hata kuitumikia timu yake ya taifa ya Kenya, Harambee Stars kwenye fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), lakini kwa sasa amepona na ameanza mazoezi na wenzake.
Wanachama na mashabiki wa timu hiyo wamekuwa na hamu ya kumuona mchezaji huyo mwenye kipaji na uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira, changa za maudhi na mbio, akimudi kucheza winga zote mbili na mshambuliaji msaidizi, namba 10.
“Alisajiliwa akiwa na majeraha, pamoja na kuwa hivyo, lakini kocha Fadlu Davids, alivutiwa mno na uwezo wake, akaamuru aasajili ili akipona aidie Simba. Ni kweli alipona, lakini jopo la madaktari waliamua apone vizuri kwa asilimia 100, ndiyo maana watu hawajamuona, lakini kwa sasa yupo tayari chini ya kocha Pantev,” alisema Ahmed.
Bajaber, ndiye mchezaji pekee aliyesajiliwa msimu huu ambaye hajaonekana uwanjani mpaka sasa, tangu mchezo wa kwanza wa kilele cha Simba Day dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, hadi wa mwisho wa Ligi Kuu, ilipocheza dhidi ya Namungo FC.
Wakati hayo yakiendelea, klabu hiyo imewataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo wasibabaishwe na cheo cha Meneja Mkuu, walichompa mwalimu wao, Pantev, badala ya Kocha Mkuu.
Ahmed, alisema cheo cha Meneja Mkuu ni kikubwa zaidi kuliko Kocha Mkuu.
“Unapokuwa Kocha Mkuu, kazi yako ni kocha tu kusimamia kuongoza mazoezi, na kuongoza mechi tu, lakini Meneja Mkuu huwa anakuwa kocha, anasajili, anatoa mapendekezo, ina maan ndani ya umeneja kuna ukocha pia.
Kwa maana huyo si kila kocha anaweza kuwa meneja, ila meneja pia anaweza kuwa kocha, hiyo ndiyo tofauti iliyopo baina yao,” alisema Ahmed.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa Simba imempa cheo hicho ili kukwepa mwalimu huyo kutokaa kwenye benchi kutokana na kutokidhi vigezo vya kuwa Kocha Mkuu, hasa kwenye michezo ya kimataifa.
Klabu hiyo imewaambia wanachama na mashabiki wake kuwa kilichowavutia kumchukua kocha huyo licha ya maneno mengi kusemwa ni sifa yake, pamoja na uwezo aliouonyesha akiwa na timu ya Gaborone United.
“Kilichotuvutia, ndiyo kocha pekee aliyechukua ubingwa mara mbili mfululizo kwenye nchi tofauti. Alichukua ubingwa nchini Cameroon, akiwa na Victoria United, 2023/24, tena akitoka kuipandisha daraja, msimu unaofuata, 2024/25, aliipa ubingwa Gaborone United, mwalimu wa namna hii siyo wa kumchukulia poa.
“Tukaangalia tulivyocheza naye. Gaborone United ni timu ndogo mno, lakini tulipokutana, sisi ndiyo tulikuwa Gaborone Unted na wao ndiyo walikuwa Simba, aliyefanya mabadiliko haya ni yeye, hivyo tukaona huyu kocha anatufaa,” alisema Ahmed.
Simba itacheza dhidi ya Nsingizini Hotspurs, Oktoba 19, mwaka huu.
The post HUU HAPA UKWELI KUHUSU BAJABER….SIMBA WAKIRI KUINGIA ‘CHA KIKE’….FADLU ATAJWA…. appeared first on Soka La Bongo.