Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Morocco imeandika historia baada ya kutwaa taji la Kombe la Dunia la Vijana (FIFA U-20 World Cup) kwa mara ya kwanza, ikipata ushindi wa mabao 2–0 dhidi ya Argentina katika mchezo wa fainali uliopigwa Jumapili.
Shujaa wa pambano hilo alikuwa mshambuliaji Yassir Zabiri, aliyetikisa nyavu mara mbili katika dakika ya 12 na 29, akiiongoza Morocco kutwaa ubingwa huo wa kihistoria. Ushindi huo umeifanya Morocco kuwa taifa la kwanza kutoka Afrika kushinda taji hilo tangu Ghana ilipofanikiwa mwaka 2009.
Argentina, ambayo ilikuwa haijapoteza mchezo wowote hadi kufika fainali, ilikosa huduma ya nyota wake wawili muhimu Claudio Echeverri wa Bayer 04 Leverkusen na Franco Mastantuono wa Real Madrid CF — hali iliyochangia kuporomoka kwao katika mchezo wa mwisho.
Safari ya Morocco kuelekea ubingwa ilikuwa ya kuvutia. Walimaliza hatua ya makundi wakiwa vinara baada ya kushinda dhidi ya Uhispania, Brazil na Mexico, kisha kuiondosha Korea Kusini katika hatua ya 16 bora, Marekani robo fainali, na Ufaransa nusu fainali kabla ya kuhitimisha kazi kwa kuivunja Argentina katika fainali.