VILLARREAL: MSHAMBULIAJI wa Manchester City, Erling Haaland, ameendeleza rekodi yake tamu ya kufunga katika kila mechi ndani ya mechi 12 mfululizo baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Villarreal kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumanne usiku.
Haaland ilikipatia kikosi cha Pep Guardiola bao la kuongoza dakika ya 17, baada ya Rico Lewis kuweka mpira ndani ya eneo la hatari na Haaland kufunga kwa shuti kali la ‘first touch’ mita chache mbele ya lango.
Bao hilo liliendeleza rekodi yake ya kufunga bao kwenye kila mechi ndani ya mechi 12 mfululizo na kufikisha mabao manne kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Bernardo Silva pia aliingia kwenye orodha ya wafungaji kwa bao la pili katika mchezo huo uliotawaliwa na wageni wa uwanja wa La Ceramica, huku ubora na upana wa kikosi cha Man City vikidhihirika wazi, na Haaland akiendelea kuongoza safu ya ushambuliaji kwa ustadi mkubwa.
Manchester City ilikaribia kupata bao la mapema sekunde chache baada ya filimbi ya kwanza, wakati Jeremy Doku alipopiga shuti la chinichini lililookolewa vyema na kipa wa Villarreal, Luiz Junior.
Kwa sasa, ni Harry Kane wa Bayern Munich pekee (mabao 19) aliyefunga zaidi miongoni mwa wachezaji wa klabu kubwa barani Ulaya, huku Haaland akiwa na mabao 15 sawa na Kylian Mbappé wa Real Madrid.
The post Haaland mwendo mdundo Ulaya first appeared on SpotiLEO.