LONDON: KOCHA wa Ajax Amsterdam, John Heitinga, amesema timu yake itakabiliana na Chelsea kwa heshima lakini bila uoga, licha ya kikosi chake kuanza vibaya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) msimu huu.
Ajax wamepoteza michezo yao miwili ya kwanza ya UCL wakifungwa 2-0 nyumbani na Inter Milan na kisha kubagazwa mabao 4-0 dhidi ya Marseille, hali ambayo imewafanya wengi kuamini kuwa watakuwa wepesi kwa Chelsea katika mchezo wa leo Jumatano usiku utakaopigwa ugenini Stamford Bridge.
“Naifahamu vyema Ligi Kuu ya England. Najua nguvu na udhaifu wa Chelsea. Ni timu yenye kasi kubwa, nguvu nyingi, na inaweza kubadilika haraka ajabu inapokuwa kwenye nafasi lakini hilo haliniogopeshi” – amesema Heitinga.
Kocha huyo, ambaye awali aliwahi kuwa kocha msaidizi wa mabingwa watetezi wa EPL Liverpool na West Ham, aliongeza kuwa ubora wa Chelsea unaonekana hadi kwa wachezaji walioko benchi.
“Jorrel Hato, aliyekuwa mmoja wa wachezaji wetu bora msimu uliopita (Ajax), sasa yupo Chelsea lakini mara chache hupata nafasi ya kucheza. Hilo pekee linaonyesha ubora wao,” aliongeza.
Licha ya presha kutoka kwa mashabiki kutokana na matokeo duni, Heitinga amesema Ajax hawataingia uwanjani wakiwa wamejiandaa kushindwa bali watabadilika na kuwaendesha Chelsea kadri wawezavyo. Pia amesisitiza kuwa anao mpango kabambe wa kuwafunga mabingwa hao wa Dunia.
Ajax kwa sasa wanashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ya Eredivisie ya Uholanzi wakiwa na pointi tisa nyuma ya vinara Feyenoord, baada ya kupoteza 2-0 dhidi ya AZ Alkmaar wikiendi iliyopita.
The post Kocha Ajax ‘aitishia nyau’ Chelsea first appeared on SpotiLEO.