NAIROBI: KAMPUNI ya huduma za matukio na teknolojia ya sauti, Xpose, imewekeza kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya Shilingi milioni 19.3 kununua ‘mixer’ ya kisasa ya sauti aina ya DiGiCo Quantum 338, ikiwa ni hatua ya kuboresha viwango vya utoaji wa sauti katika matamasha na burudani ya moja kwa moja yatakayofanyika nchini Kenya.
Kifaa hicho, ambacho kinatajwa kuwa miongoni mwa mixer bora zaidi duniani, kimetumika katika ziara za kimataifa za wasanii wakubwa akiwemo Beyoncé, Coldplay na Burna Boy.
Ujio wake nchini Kenya unachukuliwa kama hatua kubwa katika historia ya uhandisi wa sauti, sekta ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto za ubora hafifu wa sauti katika matukio makubwa ya burudani.
Kwa miaka mingi, wapenzi wa muziki wamekuwa wakilalamika kuhusu sauti kupinduka, midundo ya bass kuzidi kiwango, na ucheleweshaji wa maonesho, mambo yaliyokuwa yakiharibu uzoefu hata katika matamasha ya hadhi ya juu.
Ili kusherehekea uzinduzi wa kifaa hicho, Xpose iliandaa warsha maalum ya siku nne katika International Christian Centre (ICC), ikiendeshwa na wahandisi wa sauti wanaotambulika kimataifa wakiwemo Jason ‘Redz’ Reynolds, Anthony Torres, Veer Dhaniram, na Brandon Blackwell ambao wamewahi kufanya kazi na msanii Lauryn Hill, Alicia Keys, Shaggy, na Stephen Marley.
The post Milioni 19.3 zanunua kifaa cha kisasa cha kusimamia sauti Kenya first appeared on SpotiLEO.


