NEWCASTLE: KLABU ya Newcastle United imeendeleza mwendo wake mzuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kwa kushinda mchezo wa tatu mfululizo, baada ya kuilaza Athletic Bilbao kwa mabao 2–0 Jumatano, wapinzani wao wakiandamwa na majeraha.
Beki wa England Dan Burn alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 11 kwa kichwa safi kilichopinda kwa ustadi, kabla ya Joelinton kuongeza bao la pili mwanzoni mwa kipindi cha pili kupitia kichwa kingine kizuri, na kuiwezesha Newcastle kupanda hadi nafasi ya nane kwenye msimamo kwa pointi tisa.
Athletic, ambao walikuwa bila wachezaji nane wa kikosi cha kwanza akiwemo kiungo wa kimataifa wa Hispania Nico Williams, bado waliwasumbua vijana wa Eddie Howe. Adama Boiro alipiga shuti kali lililogonga mwamba muda mfupi baada ya bao la Burn, huku Unai Gomez naye akiwanusurisha.
Baada ya mechi nne, Athletic wamejikusanyia pointi tatu pekee, na watalazimika kujitathmini na kutafuta njia bora za kuboresha kiwango chao kujinusuru na hatihati ya kukosa nafasi kwenye hatua ya 16 bora ya michuano hiyo yenye mvuto wa kipekee duniani.
Newcastle, ambao walianza kampeni yao kwa kupoteza dhidi ya Barcelona, wamejikusanya haraka na kurudi kwa kishindo kwa kuifunga Union Saint-Gilloise, Benfica, na sasa Athletic Bilbao, kwa jumla ya mabao 9–0 mafanikio ambayo hawajawahi kuyapata tangu msimu wa 2002–03.
Kocha Eddie Howe amesema ameridhishwa na matokeo hayo:
“Nimefurahishwa sana na ushindi wa leo. Ulikuwa muhimu kuinua tena morali ya kikosi baada ya kipigo kutoka kwa West Ham wikiendi iliyopita. Hatukuwa bora sana, lakini tumetengeneza nafasi nzuri kwenye michuano hii,” amesema Howe.
Baada ya mapumziko ya kupisha kalenda ya kimataifa, Newcastle watasafiri hadi jijini Marseille nchini Italia kuvaana na wababe Olympique de Marseille, huku Athletic Bilbao wakipambana na Slavia Prague.
The post Newcastle ya UCL balaa! first appeared on SpotiLEO.



