DODOMA: NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwanafa’, amesema msiba wa msanii wa uchekeshaji Emanuel Mathias ‘MC Pilipili’ umewaunganisha watu kutoka makundi mbalimbali na kuwa ukumbusho wa thamani ya maisha.
Akizungumza katika ibada ya kumuaga msanii huyo iliyofanyika kwenye Viwanja vya Chinangali, Dodoma leo, Mwanafa alisema kifo cha MC Pilipili kimetumika kuwaonya Watanzania kuhusu maisha wanayoishi na umuhimu wa kuishi kwa wema na kumcha Mungu.
“Kilichotukutanisha hapa ni ukumbusho kwamba maisha tuliyonayo si ya kudumu. Kifo kinapaswa kuwa fundisho tosha. Ukijua kuwa ipo siku utakufa, inakufanya uishi maisha ya kumcha Mungu, kuwa na radhi zake na kutokukanyaga wanadamu wenzako,” alisema.
Mwanafa aliongeza kuwa MC Pilipili alikuwa mtu wa watu na amekuwa kiungo kati ya marafiki na wadau wengi, jambo linalodhihirisha upendo aliokuwa nao katika jamii.
“Wakati mwingine hatusemi wazi tunavyowapenda ndugu zetu, lakini wanapotuacha, ndipo tunagundua walivyokuwa mioyoni mwetu. Msiba huu utukumbushe kuishi vizuri, kutoharibiana na kukwepa kukanyagana vichwani,” alisema.
Aidha, alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Mtumba na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, pamoja na wote waliosimamia msiba, akiahidi kushirikiana kuhakikisha watoto wa MC Pilipili wanaendelea kupata elimu bila kukosa chochote.
“Ninawahakikishia, kwenye hili tutashirikiana kuhakikisha watoto wa MC Pilipili hawakosi elimu. Akili za kwenda shuleni wanazo, kinachohitajika ni ushirikiano wetu,” alisema.
Mwanafa alihitimisha kwa kusisitiza kuwa maisha yana mwisho na kila mtu anatakiwa kuishi kwa namna itakayomuacha na kumbukumbu nzuri duniani
The post Mwanafa: Kifo cha MC Pilipili kitukumbushe wema first appeared on SpotiLEO.




