LONDON: MSHAMBULIAJI wa Chelsea na timu ya taifa ya England, Cole Palmer, atakosa mechi mbili zaidi za Premier League pamoja na mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona wiki ijayo baada ya kuvunjika kidole cha mguu, kocha Enzo Maresca amethibitisha.
Palmer, mwenye umri wa miaka 23, alikuwa amerejea mazoezini hivi karibuni baada ya kuwa nje kwa takriban miezi miwili kutokana na jeraha la misuli ya nyonga, lakini safari hii majeraha yamemkumba akiwa nyumbani. Inadaiwa alijigonga kidole kwenye mlango usiku, na kufanya apate hitilafu hiyo ndogo inayohitaji muda.

Kwa mujibu wa Maresca, mshambuliaji huyo hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachosafiri kucheza na Burnley Jumamosi, wala mchezo wa nyumbani dhidi ya Barcelona Jumanne, sambamba na mechi ya wiki ijayo dhidi ya vinara Arsenal.
“Hakutakuwa tayari kwa kesho, hawezi kucheza dhidi ya Barcelona, na pia si kwa Arsenal. Ni ajali tu ya nyumbani, kajigonga kidole. Si jeraha kubwa, lakini hatarudi ndani ya wiki hii.” alisema Maresca
Palmer, aliyefunga bao mbili wakati Chelsea wakitwaa Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Paris Saint-Germain mwezi Julai, anatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha England kuelekea Kombe la Dunia mwakani.
The post Palmer kukosa mechi mbili zaidi first appeared on SpotiLEO.





