MANCHESTER: KLABU ya Bayer Levekusen ya Ujerumani imevuruga rekodi ya Manchester City ya kucheza mechi 23 za nyumbani kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya bila kupoteza baada ya kipigo adimu cha mabao 2-0 jana Jumanne.
Kipigo hicho kimeharibu sherehe ya mechi ya 100 ya Pep Guardiola kama kocha wa Man City kwenye Champions League, na kuwaacha mabingwa hao wa zamani wa England wakishika nafasi ya sita kwa alama 10 baada ya kucheza mechi tano. Alejandro Grimaldo na Patrik Schick ndio waliowafungia Leverkusen, ambao wapo nafasi ya 13.
Guardiola aliwapa mapumziko wachezaji wake wengi wa kikosi cha kwanza katika kipindi cha kwanza kwa kufanya mabadiliko 10 ya kikosi kilichocheza dhidi ya Leverkusen, uamuzi ambao uliishia kwenye kipigo hicho.
Manchester City ilikuwa ikitafuta kurekebisha mwenendo wao baada ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Newcastle United kwenye Premier League Jumamosi, lakini haikuwezekana kikwazo akiwa ni golikipa wa Wajerumani hao Mark Flekken.
Mlinda mlango huyo Mholanzi alifanya kazi kubwa kuwakosesha mabao Nathan Aké na Tijjani Reijnders, huku Man City wakiliandama lango la wageni hao kwa mashuti 20, saba yakiwa yamelenga, ikilinganishwa na mawili tu ya Leverkusen.

“Ni hisia nzuri kushinda kwenye Uwanja wa Etihad, kiukweli, Tulihitaji umoja na nguvu zetu zote kwenye mchezo huu, mapambano na uthabiti mkubwa”
“Tunajua wana ubora wa kiwango cha juu duniani, na hata wachezaji walioanza leo (jana) ni wachezaji wa daraja la juu wanaochezea timu zao za taifa. Tulijua itakuwa kazi ngumu, lakini tumefurahi kupata ushindi.” – beki wa Leverkusen Jarell Quansah ameiambia TNT Sports.
Kocha wa klabu hiyo pia, Kasper Hjulmand, amesema ulikuwa usiku wa kukumbukwa.
“Tuna furaha sana kwa ushindi huu, lakini zaidi ni tabia iliyoonesha timu. Ninawaheshimu sana wachezaji wangu. Tunajenga timu hapa, na nafikiri usiku huu utabaki kuwa sehemu ya kutupa nguvu zaidi katika safari yetu.”
The post Leverkusen yavuruga rekodi ya Man City Etihad first appeared on SpotiLEO.









