AZAM FC kwa sasa vichwa viko chini wakiuguza maumivu ya kupoteza mechi mbili za kwanza za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini mashabiki wa klabu huenda wakatuliza presha kutokana na kauli iliyotolewa na kocha mkuu, Florent Ibenge akisema watulie kwa kuwa watafikia ubora wanaotakiwa kuwa nao.
Azam inayoshiriki makundi ya CAF kwa mara ya kwanza kama ilivyo kwa Singida Black Stars, ipo Kundi B na ilianza na kichapo cha 2-0 kutoka kwa AS Maniema ya DR Congo kabla ya wikiendi iliyopita kulala tena 1-0 kwa Wydad Casablanca ya Morocco. Kundi hilo pia lina Nirobi United ya Kenya itakayocheza mechi mbili mfululizo zijazo dhidi ya Azam mapema mwakani.
Akizungumza Ibenge alisema Azam bado iko salama katika hatua za kukua kwao, ambapo licha ya kupoteza mechi mbili za awali, matokeo hayo yatawajenga wachezaji wa kikosi hicho.
Ibenge alisema Azam haiwezi kufikia malengo yake ya kuwa klabu kubwa Afrika kwa kutumia msimu mmoja, na kwamba wataendelea kupitia hatua sahihi za ukuaji bila presha wala kuangalia wanapoanguka.
“Hakuna asiyeumizwa na matokeo mabaya, lakini kama unazingatia malengo na nini mlifanya kwenye mechi hizi mbili, ukiwa na timu ambayo ndiyo kwanza inacheza hatua kubwa kama hii unafurahishwa na juhudi za wachezaji wako,” alisema Ibenge na kuongeza;
“Azam FC haiwezi kuingia makundi kwa mara ya kwanza na kuchukua ubingwa, tutapita njia kama hizi za ukuaji ili tufike kuwa wakubwa zaidi kwa ubora uwanjani.
“Unakumbuka mara ya kwanza tulikuwa na malengo ya kufika makundi, hili lilipita na sasa tunaangalia nini tutakipata hapa kwenye makundi, lakini hatutakuwa kama tulivyocheza hivi kwenye mechi zinazokuja au hata msimu ujao. Naamini wachezaji wangu wamejifunza.”
Azam usiku wa leo itakutana na Singida Black.
Hii ni mechi ya kiporo cha Ligi Kuu Bara kabla ya Jumapili kukabiliana na Simba kwenye pambano la Mzizima Derby la ligi hiyo pia.
The post BAADA YA KUPIGWA MECHI 2 CAF….IBENGE AWAPA UKWELI MCHUNGU AZAM FC… appeared first on Soka La Bongo.


