DAR ES SALAAM: MASHINDANO ya Miss World Tanzania yamerudi kwa sura mpya baada ya kampuni ya 361 Degrees Africa kuzindua rasmi mwongozo mpya wa uendeshaji unaoangazia kwa kiasi kikubwa dhana ya “Urembo wenye Malengo.”
Mashindano Hayo yanalenga kuinua hadhi ya mashindano haya nchini pamoja na kutoa nafasi pana zaidi kwa vijana wa kike kuonyesha vipaji, uongozi na ubunifu wao katika kuchangia maendeleo ya jamii.
Akizungumza na Spoti leo, Mkurugenzi wa Kitaifa wa Miss World Tanzania, Mustafahassanali, alisema dhamira ya msimu huu ni kuhakikisha urembo unatumika kama chachu ya ustawi wa jamii.
“Miss World Tanzania si shindano tu, ni safari ya kubadilisha maisha ya vijana wa kike nchini. Tunahitaji mrembo atakayeleta mabadiliko chanya kupitia miradi ya kijamii,” amesema.
Kwa mara ya kwanza, mashindano haya yataendeshwa kwa ushirikiano na Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), hatua inayolenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na kutoa fursa sawa kwa washiriki kutoka maeneo yote ya Tanzania.
Kampuni ya 361 Tanzania imeahidi kuongeza nguvu katika uratibu, mawasiliano na maandalizi ya mashindano, huku ikisisitiza kuwa msimu huu utatoa jukwaa kwa warembo wenye vipaji mbalimbali kuwakilisha nchi katika ngazi ya kimataifa.
Uzinduzi huu unaashiria ukurasa mpya katika historia ya Miss World Tanzania ukurasa unaoipa kipaumbele thamani ya utu, ubunifu na mchango halisi wa warembo katika maendeleo ya taifa.
The post Miss World Tanzania Yarudi Upya first appeared on SpotiLEO.




