WAKATI kikosi cha Singida Black Stars kikitarajiwa kushuka uwanjani kesho jioni kuvaana na TRA United, zipo taarifa kuwa kiungo wa timu hiyo, Khalid Aucho yupo katika rada za wababe wa Morocco, Raja Athletic wanaonolewa na kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids.
Aucho alijiunga na Singida kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Yanga alikokuwa amecheza kuanzia 2021-2025. Msimu wa 2023/24 alicheza mechi 20 kwa dakika 1629 akitoa asisti mbili, 2024/25 alifunga bao moja dhidi ya Mashujaa ambao Yanga ikishinda 5-0.
Chanzo kimedai endapo kama Aucho atafanikiwa kujiunga na Raja Athletic ataungana na Fadlu, kocha ambaye wakati akiwa Simba, Aucho alikuwa anakipiga upande wa pili kwa watani, Yanga.
“Kocha Fadlu ndiye anayemhitaji Aucho na mazungumzo yanaendelea na ofa aliyowekewa mezani ni nono ingawa siwezi kusema ni kiasi gani,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Aucho amebakiza mkataba wa miezi sita anaruhusiwa kuzungumza na timu zingine kwa kuzingatia taratibu zinazotakiwa ikiwemo kuzungumza na viongozi wa SBS.”
Alipotafutwa ili kuzungumzia jambo hilo, Fadlu amesema kuhusu kuhitaji huduma ya kiungo huyo hilo hawezi kulizungumzia kwa sababu ni mchezaji mwenye mkataba na timu nyingine, lakini akakiri kwamba ni miongoni mwa wachezaji wenye uwezo mkubwa uwanjani.
“Aucho ni mchezaji mwenye maarifa makubwa uwanjani, anatumia akili kubwa kuhakikisha timu haichezi na presha ni miongoni mwa wale ninaowakubali katika Ligi Kuu ya Tanzania,” amesema Fadlu aliyeiwezesha Simba kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kupoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-1.
The post AUCHO KWENYE RADA ZA KOCHA WA SIMBA…OFA NONO YAWEKWA MEZANI…. appeared first on Soka La Bongo.







