BOURNEMOUTH: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca, amesema ni lazima wafanye ‘rotation’ ya wachezaji ili kuwalinda wale wasioweza kucheza kila baada ya siku tatu, timu ikijiandaa na safari ya kuelekea Bournemouth baada ya kupoteza 3-1 dhidi ya Leeds United Jumatano.
Maresca alikosolewa vikali kufuatia kichapo hicho kutoka kwa Leeds wanaopambana kuepuka kushuka daraja, ambapo alifanya mabadiliko matano kwenye kikosi kilichotoka sare ya 1-1 dhidi ya vinara Arsenal licha ya Chelsea kucheza pungufu ya mchezaji mmoja mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kipigo hicho kilikatisha rekodi ya Chelsea ya kutopoteza mechi saba mfululizo kwenye mashindano yote. The Blues wanaoshika nafasi ya nne wako pointi tisa nyuma ya Arsenal.
“Sababu kubwa ya mabadiliko ya wachezaji tunaoufanya ni kwamba kuna wachezaji hawawezi kucheza kila baada ya siku tatu. Tuna wachezaji wanne au watano tunaotakiwa kuwalinda na kuwasimamia,”
“Natamani ningemchezesha Reece (James), Pedro (Neto), Moi (Moises Caicedo), hata Romeo (Lavia) kwenye kila mchezo, lakini haiwezekani. Tunajaribu kutafuta suluhisho tofauti.” – Maresca amewaambia waandishi wa habari.

Mchezo wa Jumamosi dhidi ya Bournemouth utakuwa wa tano ndani ya wiki mbili tangu kumalizika kwa mapumziko ya kimataifa. Moises Caicedo, aliyepangwa kwenye mechi 50 kati ya 51 chini ya Maresca, ataendelea kukosekana kwa mechi mbili zaidi huku akimalizia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu. Lavia, Levi Colwill na Dario Essugo wote ni majeruhi.
“Nimeangalia tena mechi dhidi ya Leeds. Tulikosea mambo mengi. Tulilipa gharama kwa sababu ugenini kwa Leeds kunaweza kuwa kugumu. Kuna mambo tunapaswa kuyaepuka baadaye,” ameongeza.
Kocha huyo aliongeza kuwa anatarajia mechi ya Bournemouth kuwa na mwelekeo uleule wa mchezo wa Leeds.
“Leeds walikuwa na ‘intensity’ kubwa na walituzidi katika karibu kila eneo. Natumai tumejifunza na tutakuwa bora kesho,” alisema.
The post Maresca aanika sababu za kufanya ‘rotation’ first appeared on SpotiLEO.







