BAMAKO: KOCHA wa timu ya Taifa ya Mali, Tom Saintfiet, amesema soka la Afrika linastahili kuheshimiwa zaidi, baada ya hatua ya ghafla ya FIFA kuchelewesha muda wa kuachiliwa kwa wachezaji kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika baadae mwezi huu nchini Morocco.
FIFA ilitangaza Jumatano kwamba klabu zitalazimika kuachia wachezaji kuanzia Desemba 15 pekee wiki moja nyuma ya dirisha la kawaida la kimataifa hatua iliyokuja takribani wiki tatu kabla ya kuanza kwa mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Desemba 21 hadi Januari 18.
Mashindano ya 35 ya AFCON yalipangwa awali kufanyika wakati wa kiangazi cha Kaskazini ili kuepuka migongano na ligi za Ulaya, lakini yakahamishwa kwenda msimu wa baridi kutokana na sababu za hali ya hewa.

Akizungumza na Reuters kwa njia ya mtandao, Saintfiet amesema dunia inapaswa kutambua ukubwa wa soka la Afrika na kuliheshimu. Kuhusu muda mwafaka wa kuandaa mashindano hayo, alisisitiza kuwa hakuna kipindi ambacho huwa kamilifu kwa kila upande.
“Ukisema ni katikati ya msimu, unafikiria Ulaya Magharibi, lakini wao si watawala wa soka la dunia wachezaji wanaocheza Norway, Sweden, Finland, Iceland, Ireland na Russia huwa wanamaliza msimu wakati huo, hivyo dunia isijikite tu kwenye England, Ujerumani au Italia,” – amesema.
“Afrika inapaswa kufanya kile kinachofaa kwao, hasa kwa kuzingatia hali ya hewa. Dunia inapaswa kuanza kuikubali Afrika”.

Saintfiet alikumbusha kuwa mashindano kama Kombe la Dunia pia husababisha ligi kadhaa kusimama, hivyo AFCON haipaswi kuonekana kama kikwazo cha kipekee.
Uamuzi wa FIFA umeilazimu Mali kufuta michezo ya kirafiki waliyopanga kabla ya mechi yao ya kwanza dhidi ya Zambia tarehe 22 Desemba, wakifuatiwa na wenyeji Morocco na Comoros katika Kundi A.
The post “Soka la Afrika linastahili heshima” – kocha wa Mali first appeared on SpotiLEO.








