Azam FC yaizuia Simba kusonga mbele
SIMBA imejikuta ikishindwa kuvuna alama tatu muhimu mbele ya Azam FC katika mchezo wa Mzizima Derby, baada ya kukubali kichapo cha bao 2-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mchezo huo uliovuta hisia za mashabiki ulianza kwa kasi ya juu, huku kila upande ukionesha kiu ya kupata ushindi.
Katika dakika za mwanzo, Simba ndiyo iliyoonekana kuingia vizuri zaidi kwenye mchezo, ikimiliki mpira na kushambulia kwa kasi.
Licha ya kutengeneza nafasi kadhaa za hatari ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, mashambulizi yao hayakuzaa matunda kutokana na umakini hafifu katika eneo la mwisho.
Dakika ya 23, Joshua Mutale alipata nafasi mwendo wa hatari lakini shuti lake lilikwenda nje, na kuwaacha mashabiki wa Simba wakishika vichwa.
Hali hiyo haikubadilika hata dakika ya 34, baada ya kipa wa Azam FC, Zuberi Foba, kuokoa mpira wa faulo uliopigwa na Elie Mpanzu kwa ustadi mkubwa.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa sare tasa ya 0-0, licha ya Simba kuonekana kutawala mchezo na kutengeneza nafasi nyingi zaidi. Mara tu kipindi cha pili kilipoanza, Simba iliendelea kusukuma mashambulizi, huku mpira mmoja ukigonga mwamba dakika ya 47 na kuendeleza bahati mbaya kwa wekundu hao.
Azam FC waliibuka na nguvu mpya katika dakika za mwisho za mchezo, wakitumia makosa ya Simba kusaka ushindi. Dakika ya 81, Japhte Kitambala aliifungia Azam FC bao la kwanza akimalizia kazi nzuri ya Nassor Saadun, bao lililobadili kabisa mwelekeo wa mchezo.
Dakika nane baadaye, Iddi Nado alizidi kuzamisha jahazi la Simba baada ya kufunga bao la pili dakika ya 89, na kuipa Azam FC uongozi wa 2-0 uliodumu hadi dakika ya mwisho. Bao hilo liliwatia nguvu vijana wa Chamazi waliocheza kwa nidhamu na umakini mkubwa.
Kwa matokeo hayo, Simba imepoteza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara tangu kuanza kwa msimu wa 2025/2026. Upande wa pili, Azam FC imejihakikishia alama tatu muhimu, ikiwa ni ushindi wao wa pili katika michezo mitano ya ligi msimu huu.
The post SIMBA SC IMELAZWA CHALI NA AZAM FC KWA MKAPA appeared first on Soka La Bongo.






