KOCHA mkuu wa Yanga, Pedro Gocalves , ameibuka na kufunguka juu ya kiwango cha mshambuliaji wake, Prince Dube, amesema kuwa bado anamwamini lakini sasa anamwekea jukumu zito la kuhakikisha anakuwa mhimili wa safu ya ushambuliaji msimu huu.
Pedro amesema kuwa Dube ameonyesha dalili nzuri, lakini bado anatakiwa kuongeza uthabutu na uthabiti katika mechi kubwa.
“Dube ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na uwezo wa kufanya maamuzi ya haraka ndani ya boksi, jambo ambalo lilionekana katika mchezo na Coastal Union alifunga bao muhimu,” amesema.
Kocha huyo amesisitiza kuwa uwezo huo unapaswa kuonekana mara kwa mara, hasa katika mechi ngumu zinazohitaji utulivu na ubunifu wa hali ya juu.
Ameongeza kuwa moja ya sababu zinazomfanya amtegemee Dube ni namna anavyojituma mazoezini na hamasa ya kutaka kufikia kiwango bora zaidi, ushindani ndani ya kikosi umeongezeka hivyo kila mchezaji anapaswa kupigania namba kwa nguvu zote.
Pedro amesema anapenda kuona Dube akiongeza idadi ya mabao, kuwa mshambuliaji wa kiwango chake anatakiwa kufunga mara kwa mara na sio kutegemea mechi chache kuonyesha ubora.
Ameweka wazi kuwa msimu huu Yanga inataka kumaliza ligi bila kuwa na presha, jambo litakalowezekana ikiwa washambuliaji watawajibika ipasavyo.
Kocha huyo pia amezungumzia changamoto ambazo Dube amekuwa akipitia, ikiwemo majeraha ya mara kwa mara yaliyowahi kumrudisha nyuma.
Ameeleza kuwa timu ya benchi la ufundi imekuwa ikifanya kazi kubwa kuhakikisha anamrejesha kwenye ubora na kumjengea utulivu wa kimwili na kiakili.
Pedro amesisitiza kuwa nafasi ya kucheza haipo kwa jina, bali kwa kile mchezaji anachokifanya uwanjani. amemtaka Dube asipunguze kasi wala kuridhika na kiwango alichokionyesha wiki iliyopita, bali aongeze njaa ya mafanikio na kuwa mfano wa kuigwa kwa washambuliaji wengine.
Pedro ameweka wazi kuwa kama Dube atatimiza mahitaji yake ya kiufundi na kuongeza makali, ataendelea kuwa silaha muhimu ya Yanga msimu huu.
The post DUBE KUBEBESHWA MAJUKUMU MAZITO, PEDRO ASEMA appeared first on Soka La Bongo.





