KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua, ameangukia panga baada ya kuachwa kwenye kikosi cha mwisho cha Ivory Coast kitakachoshiriki AFCON 2025, licha ya kiwango kikubwa alichokionesha akiwa na Wananchi msimu huu.
Uamuzi huo umewaacha mashabiki wengi wakishangaa, hasa ikizingatiwa namna ambavyo amekuwa mhimili wa ubunifu katika kikosi cha Yanga.
Kocha Mkuu wa Ivory Coast alipotangaza kikosi chake cha mwisho bila kumjumuisha Zouzoua, mitandao ya kijamii iliwaka moto. Wengi walitarajia kiungo huyo angepewa nafasi kutokana na kasi, ufanisi na mchango wake katika mabao ya Yanga kwenye Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika, ameonekana kuwa katika kiwango bora zaidi tangu ajiunge na Wananchi.
Kwa Pacome mwenyewe, hii ni pigo lisilofichika. Akiwa mhimili kwenye mfumo wa Kocha Pedro Gonçalves, amekuwa akihusika moja kwa moja na kutengeneza mabao, jambo lililomfanya kuonekana kama mmoja wa wachezaji waliokuwa na nafasi kubwa ya kuvaa jezi ya Taifa katika AFCON mwaka huu. Kutemwa kwake kumetafsiriwa na wachambuzi kama ushindani mkali uliopo katika kikosi cha Tembo wa Ivory Coast.
Hata hivyo, kocha wa Ivory Coast ameenda na kikosi chenye uzoefu mkubwa wa michuano mikubwa, jambo lililofanya ushindani wa nafasi kuwa mgumu zaidi kwa wachezaji wanaochipukia kimataifa kama Zouzoua.Mastaa waliopata nafasi wametajwa kuwa na historia ya kuaminiwa kwenye mashindano ya juu, ikiwamo fainali za AFCON zilizopita.
Pacome aliwahi kuitwa katika kikosi cha Ivory Coast mwezi Oktoba, kwa ajili ya michezo ya kirafiki dhidi ya Seychelles na Kenya, hali iliyowafanya mashabiki kuamini kuwa alikuwa anajengewa mazingira ya kuwa sehemu ya kikosi cha AFCON. Lakini safari yake safari hii imekatishwa kwa hatua ya mwisho.
Kikosi kilichotangazwa kimejumuisha makipa Yahia Fofana, Mohamed Koné na Alban Lafont, huku safu ya ulinzi ikiwa na majina kama Emmanuel Agbadou, Willy Boly, Ousmane Diomandé, Guela Doué na Ghislain Konan. Hii ni safu iliyojaa mawe ya zamani na vijana wanaong’ara Ulaya.
Katika kiungo na ushambuliaji, wameitwa Odilon Kossounou, Evan Ndicka, Seko Fofana, Jean-Philippe Gbamin, Franck Kessié, Ibrahim Sangaré na Jean-Michael Seri, huku mbele kukiwa na mastaa kama Amad Diallo, Sébastien Haller, Wilfried Zaha, Oumar Diakite na Jean-Philippe Krasso.
Kwa sasa, Zouzoua atalazimika kuendelea kufanya kazi na kuonyesha kiwango chake ndani ya Yanga, akitumaini kuitwa tena siku zijazo. Mashabiki wa Wananchi wameapa kuendelea kumuunga mkono, wakiamini bado ana nafasi kubwa kwenye timu ya taifa ya Ivory Coast.
The post KIUNGO WA YANGA ATEMWA NA IVORY COST appeared first on Soka La Bongo.






