OFISA Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kikosi cha timu hiyo kimepewa mapumziko rasmi na kinatarajiwa kurejea kambini Desemba 15 mwaka huu kuendelea na maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na michuano ya kimataifa.
Kamwe amesema kuwa benchi la ufundi limetoa mapumziko kuanzia Desemba 7 hadi Desemba 15, ambapo baada ya kurejea, wachezaji wataendelea na programu maalumu hadi Desemba 20 kabla ya kupumzika tena hadi Desemba 28.
Amesema utaratibu huo umelenga kutoa muda wa wachezaji kusherehekea sikukuu na familia zao, ambapo wanatakiwa kurejea Desemba 29 tayari kwa maandalizi ya mwisho kuelekea hatua ngumu zinazowakabili.
Kwa mujibu wa Kamwe, kipindi hicho cha maandalizi ni muhimu kwa kuwa mwezi Januari Yanga itakabiliwa na ratiba ngumu yenye mechi za Ligi Kuu na zile za kimataifa, kutegemea ratiba ya mwisho itakayotolewa na Bodi ya Ligi.
Amesema lengo la programu hiyo ni kuhakikisha timu inarejea kwenye ushindani ikiwa katika hali bora, sambamba na kuhakikisha wachezaji wanaendelea kuwa katika utimamu wa juu kuelekea mashindano hayo.
Akizungumzia timu nyingine ndani ya klabu, Kamwe alisema Ligi ya Wanawake inaendelea ambapo Desemba 12 Yanga Princess watashuka dimbani kuvaana na Tausi FC kwenye Uwanja wa KMC Complex.
Kamwe aliongeza kuwa timu ya vijana ya klabu hiyo, U-20, inatarajiwa kucheza Desemba 17, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ratiba ya shughuli za mwezi mzima kwa timu zote tatu za Yanga.
The post YANGA KUNGIA KAMBINI DESEMBA 15 appeared first on Soka La Bongo.









