MADRID: KOCHA wa Girona, Míchel, amemkosoa vikali kipa wa klabu hiyo raia wa Croatia Dominik Livakovic, akidai mchezaji huyo hana uzalendo na haipi kipaumbele klabu na kusema kuwa hatachezea timu hiyo tena.
Míchel amesema kipa huyo wa akiba alikataa kucheza mechi ya hivi karibuni na ameeleza wazi kutaka kuondoka klabuni hapo, akijielekeza zaidi kwenye maandalizi ya Kombe la Dunia kuliko majukumu ya Girona.
“Livakovic ni mtu mzuri sana, lakini malengo yake hayalingani na ya Girona, anahitaji kucheza kwa ajili ya Kombe la Dunia, si Girona. Aliniambia mwenyewe. Alisema hataki kubaki, anataka kwenda timu nyingine kwa sababu akicheza Girona hataweza kucheza klabu nyingine.” – amesema Míchel.
Kwa mujibu wa Míchel, kipa huyo mwenye umri wa miaka 30, ambaye yuko kwa mkopo kutoka Fenerbahce, alikataa kucheza ili abaki na haki ya kusajiliwa na klabu nyingine, ikizingatiwa kuwa mchezaji anaruhusiwa kuchezea timu mbili tu kwa msimu na tayari alishachezea Fenerbahce.

Kocha huyo alisema alitaka Livakovic acheze mechi ya Copa del Rey mapema mwezi huu, lakini mchezaji huyo aligoma, na kumlazimisha mlinda lango wa kwanza, Paulo Gazzaniga, kucheza akiwa na homa kali.
“Kwa sasa nina kipa mmoja tu, utiifu wa Gazzaniga haujawahi kutiliwa shaka. Hadi dirisha la usajili la Januari, tunalo tatizo. Sijilindi mimi, namlinda kipa aliyekuwa nasi kwa miaka mitatu.” – ameongeza
Míchel amesema uamuzi wake wa kuweka suala hilo wazi ni kwa sababu anaamini mashabiki wa klabu hiyo wanapaswa kujua hali halisi inayoendelea kikosini hapo.
Gazzaniga, hata hivyo, amekuwa na msimu wenye misukosuko, akifanya makosa kadhaa ya kusikitisha ikiwemo katika mechi ya ufunguzi wa La Liga, na tena Jumapili iliyopita ambapo makosa yake yalisababisha mabao mawili ya Elche.
Moja lilitokana na kumpasia mpinzani moja kwa moja ndani ya boksi, na jingine baada ya kushindwa kuizuia kwa urahisi shuti lililopigwa kwenye ‘near post’.
Girona inashika nafasi ya 18 kwenye msimamo wa La Liga, ndani ya eneo la kushuka daraja.
The post Golikipa Livakovic apigwa ‘stop’ Girona first appeared on SpotiLEO.







