RASMI wa Klabu ya Yanga na Mwenyekiti wa Muungano wa Vilabu Afrika (ACA), Eng. Hersi Said, amejitokeza kutoa ufafanuzi kuhusu kauli na wasilisho lake lililozua mjadala miongoni mwa wadau wa soka, hususan likihusishwa na Klabu ya Simba.
Amesisitiza kuwa hakukuwa na nia yoyote ya kuishambulia Simba bali kulikuwa na tafsiri potofu zilizojitokeza.
Kupitia kituo kimoja cha radio, Eng. Hersi alianza kwa kuwapongeza wale waliotafuta taarifa sahihi kabla ya kutoa hitimisho, akieleza kuwa kuna watu wamekuwa wakijadili hoja bila kuelewa muktadha halisi wa kile kilichowasilishwa.
Alifafanua kuwa madai ya kuwepo kwa masimango dhidi ya Simba si ya kweli na hayakuwa sehemu ya maudhui yake.
Ameeleza kuwa wasilisho lake haikuilenga Simba kama klabu, bali ilijikita katika kuangazia maendeleo ya vilabu kwa ujumla na mabadiliko yanayohitajika ili kusukuma mbele soka la Afrika. Katika wasilisho hilo, amesema kulikuwa na maeneo matatu makuu aliyoyajadili kwa kina.
Kwa mujibu wa Hersi, eneo la kwanza lilihusu changamoto zinazovikabili vilabu vya Afrika, akibainisha kuwa changamoto hizo haziwezi kutenganishwa na mjadala wa mifumo ya uendeshaji wa vilabu. Alisisitiza kuwa alipotoa mfano wa mashabiki wa Simba, haikuwa tafsiri ya kudhalilisha au kuonyesha kuwa klabu hiyo haina uongozi mzuri.
Ameongeza kuwa zaidi hoja kuu ilikuwa ni juu ya umuhimu wa utawala bora katika kuendesha vilabu, akisisitiza kuwa ni eneo linalopaswa kupewa kipaumbele ili kuleta maendeleo endelevu. Kwa mtazamo wake, utawala bora ni tofauti na uongozi bora, ingawa mambo hayo mawili yana uhusiano wa karibu.
Katika kauli yake, Eng. Hersi ameonyesha heshima kubwa kwa viongozi wa Simba, akiwataja Mangungu na Magori kuwa ni viongozi wazuri wenye uzoefu mkubwa katika soka. Amesema mjadala unaoendelea hauwalengi watu binafsi bali unahusu mifumo na kanuni za uendeshaji wa vilabu.
Rais huyo wa Yanga aliwahimiza wadau wa soka kutafakari hoja kwa upana wake badala ya kuzichukulia kwa hisia. kuwa lengo lake ni kuona vilabu vya Afrika vinapiga hatua kupitia mabadiliko chanya ya kiutawala, jambo litakalosaidia kukuza ushindani na maendeleo ya soka barani Afrika.
The post SIKUWALENGA SIMBA, HERSI AFUNGUKA HAYA appeared first on Soka La Bongo.








