LONDON: KOCHA wa Chelsea Enzo Maresca amezima kabisa tetesi zinazomuhusisha na nafasi ya ukocha Manchester City, akisema uvumi huo haumtikisi hata kidogo na bado amejikita kikamilifu kuitumikia klabu ya Chelsea.
Maresca, ambaye aliwahi kufanya kazi kama kocha msaidizi Manchester City, alijiunga na Chelsea mwaka 2024 na mara moja akaacha alama baada ya kuiongoza klabu hiyo kutwaa taji la Europa Conference League mwishoni mwa msimu wake wa kwanza, kabla ya kuongeza Kombe la Dunia la Klabu mwezi Julai.
Ripoti ya jarida la The Athletic wiki hii ilidai kuwa kocha huyo raia wa Italia mwenye umri wa miaka 45 ni miongoni mwa wagombea wakuu wa kumrithi Pep Guardiola endapo Mhispania huyo ataamua kuhitimisha safari yake yenye mafanikio makubwa Etihad.

Akizungumzia taarifa hizo kuelekea mchezo wa Ligi Kuu England ugenini dhidi ya Newcastle United, Maresca amesema hana wasiwasi wowote.
“Haijaniathiri hata kidogo kwa sababu najua ni uvumi wa asilimia 100. Kwa sasa hakuna muda wa kufikiria mambo kama hayo, hasa kwa kuwa nina mkataba hapa hadi mwaka 2029.” – amesema Maresca.
“Nimesema mara nyingi, lengo langu ni klabu hii tu na najivunia sana kuwa hapa. Huu ni uvumi tu. Wiki iliyopita huko Italia ilikuwa Juventus, sasa ni City. Sijishughulishi nao kwa sababu najua si kweli. Kuelewa kwa nini habari kama hizi zinatoka si kazi yangu mimi sijali kabisa.” – ameongeza
Maresca pia alisisitiza kuwa bado ana malengo makubwa ya kutimiza akiwa Stamford Bridge, huku Chelsea ikiendelea na mwenendo mzuri baada ya kufuzu nusu fainali ya Kombe la Carabao kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Cardiff City Jumanne.
Kwa msimamo huo, kocha huyo ameweka wazi kuwa kwa sasa mawazo yake yako kwenye matokeo uwanjani, si tetesi za soko la makocha.
The post Maresca akanusha kuitaka Man City first appeared on SpotiLEO.






