WAKATI klabu mbalimbali barani Afrika zikiendelea kujiunga na Umoja wa Vilabu Afrika (ACA), uongozi wa Simba umeweka wazi kwamba haujawahi kushawishika kuingia kwenye umoja huo bila kufahamu kwa kina manufaa yake kwa klabu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, amesema bado hana msimamo wala maoni ya moja kwa moja kuhusu ACA, akisisitiza kuwa wanahitaji kwanza kuelewa kwa undani umoja huo ulivyoanzishwa na namna unavyofanya kazi kabla ya kufanya uamuzi wowote.
Magori amesema Simba haitachukuliwa na upepo wa hisia au ushabiki katika maamuzi yake, bali itaongozwa na maslahi ya klabu kwa ujumla, baadhi ya viongozi wa umoja huo wamekuwa hawaheshimu vilabu, jambo linalowafanya kuwa waangalifu zaidi.
“Sina maoni yoyote kwa sasa kwa sababu tunataka kujua huu umoja umeundwa vipi na unafanya kazi kwa mfumo gani. Hadi hapo, hatuwezi kusema Simba itaingia au la,” amesema Magori.
Ameongeza kuwa Simba haitafanya maamuzi kwa misingi ya kushawishika au kufuata mkumbo, bali itajiuliza maswali ya msingi kuhusu faida halisi itakayopata endapo itaamua kujiunga na umoja huo.
“Hatufanyi mambo kwa ushabiki. Tunaangalia tunapata nini na tunaingia kwa lengo gani. Hadi tujue faida zake, Simba haina maoni juu ya kujiunga na umoja huo,” amesisitiza.
Hadi sasa, klabu mbili kutoka Tanzania, Yanga na Azam FC, tayari zimejiunga na ACA, huku klabu nyingine barani Afrika zikiwemo Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Gaborone United, Al Hilal ya Sudan, Wydad AC ya Morocco, Vipers SC ya Uganda na Petro de Luanda ya Angola nazo zikiwa sehemu ya umoja huo.
The post SIMBA YAHOJI MANUFAA YA KUJIUNGA NA ACA appeared first on Soka La Bongo.




