DAR ES SALAAM:MSANII maarufu wa muziki wa Singeli, Dogo Paten, ameomba msamaha kwa mtu yeyote aliyemkosea kwa namna yoyote ile, huku akihimiza amani na upendo kuelekea mwishoni mwa mwaka.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, msanii huyo amesema kuwa kama binadamu si mkamilifu na huenda kwa makusudi au bila kukusudia aliwakwaza watu katika kipindi cha mwaka unaokaribia kuisha.
“Mwaka umekaribia kuisha, mimi ni mwanadamu si mkamilifu. Huenda kuna siku nilikusema, nilikukera, nilikuudhi au niliondoa amani moyoni mwako iwe bahati mbaya au kwa kukusudia.
Kama lipo moja katika haya, naomba unisamehe,” ameandika Paten.
Dogo Paten ameongeza kuwa huenda pia aliwahi kudanganya, kudharau au hata kuharibu siku ya mtu bila yeye kutambua, hali iliyomsukuma kuamua kuomba radhi kwa wote aliowakwaza.
Aidha, msanii huyo amesisitiza umuhimu wa kumaliza mwaka kwa amani na upendo, akisema kufanya hivyo ni njia bora ya kuukaribisha mwaka mpya kwa baraka.
“Tumalize mwaka kwa amani na upendo. Nakuombea kwa Mungu akupe kibali katika siku zilizobaki ili upate tiketi ya kuingia mwaka 2026,” aliongeza.
Hatua ya Dogo Paten imepokelewa kwa hisia chanya na mashabiki wake wengi mitandaoni, wakimpongeza kwa unyenyekevu na moyo wa kuhimiza msamaha, mshikamano na maelewano katika jamii.
The post Dogo Paten aomba msamaha kwa aliyemkosea first appeared on SpotiLEO.








