DAR ES SALAAM:MSANII wa muziki wa Singeli na Bongo Fleva, Dulla Makabila, amesema ameandika historia mpya katika kazi yake ya muziki baada ya kutumia kiasi cha Sh milioni 20 kwa ajili ya kutengeneza video ya wimbo mmoja.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, msanii huyo amesema hiyo ni mara ya kwanza kwake kutumia bajeti kubwa kiasi hicho katika video, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya ukuaji wake binafsi pamoja na kukuza tasnia ya Singeli kwa ujumla.
“Kwa mara ya kwanza nimelipa Sh milioni 20 kwa video moja, kitu ambacho ni cha kawaida sana kwa Diamond Platnumz. Ila kwa upande wetu wa Singeli, vijana wangu hali zao mnazijua, video wengine hulipa hadi laki nne na nusu, unakuta director akiona kijiwe cha bodaboda anakwambia vaa reflector,” ameandika Dulla.
Dulla ameongeza kuwa licha ya gharama kubwa, anaamini uwekezaji huo utamlipa baadaye, kwani ameuchukulia kama hatua muhimu ya maendeleo yake na ya muziki wa Singeli.
“Kwa upande wangu huu ni uwekezaji ninaoamini utanilipa. Ni hatua za ukuaji wangu na tasnia nzima ya muziki wa Singeli. Naamini hata mzee wangu Majizzo, mama yangu Zamaradi Mketema pamoja na wadau wote wa Singeli wenye nia njema watakuwa wanajivunia,” ameongeza.
Aidha, Dulla amemshukuru director Fole_x na timu yake kwa kazi kubwa waliyofanya, akisema ukubwa wa bajeti umeendana na ukubwa wa maudhui ya wimbo huo.
“Asante sana ndugu yangu Fole_x, imani yangu ni kubwa sana kwako na watu wako. Tumefanya kitu kikubwa, ukubwa wa bajeti umeendana na ukubwa wa stori ya wimbo,” ameandika.
Mwisho, Dulla aliwahimiza wasanii wengine wa Singeli kujifunza umuhimu wa uwekezaji katika kazi zao, akiwataka wale anaowaita “wasanii wa gharama nafuu” wajitokeze kujifunza.
“Naomba muwaite wasanii wa Singeli wa gharama nafuu hapo chini waje wajifunze nini maana ya uwekezaji,” ameandika Dulla Makabila.
The post Dulla Makabila awekeza Milioni 20 kwenye video first appeared on SpotiLEO.








