UONGOZI wa Klabu ya Yanga upo mbioni kuwanufaisha mashabiki wake baada ya kukamilisha mchakato wa uhamisho wa nyota wawili kutoka Singida Black Stars, Marouf Tchakei na Mohamed Damaro Camara, ambao wanatarajiwa kujiunga na kikosi hicho kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi.
Taarifa zinaeleza kuwa makubaliano kati ya Yanga na Singida Black Stars yamekamilika kikamilifu, huku maandalizi yote muhimu yakiwa yameshafanyika ili kuhakikisha wachezaji hao wanaungana na timu mapema kabla ya safari ya kuelekea Visiwani Zanzibar ambako mashindano hayo yanaendelea.
Imebainishwa kuwa Marouf na Camara wanatarajiwa kuungana na kikosi cha Yanga mapema, jambo litakalowapa muda wa kuzoea mifumo ya benchi la ufundi kabla ya kuanza kwa michezo ya ushindani katika mashindano hayo muhimu.
Licha ya Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, kutotaja majina ya wachezaji hao moja kwa moja, alithibitisha kuwa wachezaji wapya waliosajiliwa katika dirisha dogo la usajili watakuwa sehemu ya msafara wa timu unaoelekea Zanzibar.
“Tunatarajia katika safari yetu ya kwenda Zanzibar Januari 3, 2025, wachezaji wetu wapya akiwemo kiungo wa kati atakuwa sehemu ya kikosi na kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi,” amesema Kamwe.
Kamwe ameongeza kuwa suala la kupanga kikosi litakuwa jukumu la benchi la ufundi, lakini ana imani kuwa nyota wote wapya waliopo kwenye mipango ya klabu watasafiri na timu kwenda Zanzibar kwa ajili ya michuano hiyo.
Kamwe ameeleza kuwa kiungo Attohoula Yao atarejea kikosini baada ya kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha, sambamba na kurejea kwa wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu za Taifa katika michuano ya AFCON, akiwemo mshambuliaji Prince Dube, ambaye anatarajiwa kujiunga na kikosi kabla ya safari ya kwenda Zanzibar.
The post NYOTA WA YANGA MSAFARA WA KOMBE LA MAPINDUZI appeared first on Soka La Bongo.





