KIUNGO mpya wa Yanga, Marouf Tchakei, ameanza rasmi safari yake ndani ya kikosi cha Wananchi baada ya kuwa sehemu ya timu iliyowasili visiwani Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi linaloendelea kutimua vumbi.
Tchakei bado hajatambulishwa na Yanga, amesajiliwa kwa mkopo akitokea Singida Black Stars kufuatia makubaliano maalum kati ya klabu hizo mbili, hatua inayolenga kuimarisha kikosi cha timu hiyo katika kipindi hiki cha mashindano.
Nyota huyo anatarajiwa kuanza kuonekana uwanjani mapema, akitajwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza mchezo wa kesho dhidi ya KVZ, utakaopigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Ujio wa Tchakei unaongeza nguvu mpya katika safu ya kiungo ya Yanga, benchi la ufundi chini ya kocha Pedro Gocalves ana matumaini kuwa atasaidia kuongeza ushindani, ubunifu na uimara katika michezo ya mashindano yaliyopo mbele yao.
Mbali na Kombe la Mapinduzi, Yanga inamwangalia Tchakei kama sehemu ya mpango mpana wa kuhakikisha timu inafanya vizuri pia katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara pamoja na mashindano mengine ya msimu huu.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya kikosi, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema timu imeondoka ikiwa na wachezaji wote waliopo nje ya majukumu ya timu ya taifa pamoja na nyota wao wapya waliosajiliwa.
Kamwe ameeleza kuwa wachezaji wapya wataanza kuonekana katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, akisisitiza kuwa usajili uliofanywa umezingatia mahitaji ya benchi la ufundi na malengo ya muda mfupi na mrefu ya klabu hiyo.
The post MAROUF RASMI KUITUMIKIA JANGWANI appeared first on Soka La Bongo.





