KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kushuka dimbani kesho kuanza rasmi kampeni yake ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa kuikabili KVZ, mchezo utakaochezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.
Akizungumza kuelekea mchezo huo wa ufunguzi, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema maandalizi waliyoyafanya yamelenga kujenga msingi imara wa ushindani katika kila mechi watakayocheza kwenye mashindano hayo, huku akisisitiza umuhimu wa nidhamu na mshikamano wa kikosi.
Pedro amekiri kuwa kikosi chake kitakabiliwa na changamoto ya kuwakosa baadhi ya wachezaji muhimu, lakini amesema hilo halitapunguza morali wala malengo ya timu katika mashindano hayo.
Ameeleza kuwa Yanga bado ina wachezaji wa kutosha wenye uwezo wa kupambana na timu yoyote, akibainisha kuwa nguvu kubwa ya kikosi hicho ipo kwenye mshikamano, nidhamu ya mchezo na utekelezaji wa maelekezo ya benchi la ufundi.
“Kesho tunaanza rasmi mashindano haya na tumekuja kupambana kwa dhati. Ni kweli tunawakosa baadhi ya wachezaji muhimu, lakini bado tuna kikosi imara cha kushindana,” amesema Pedro.
Kocha huyo ameongeza kuwa Kombe la Mapinduzi ni jukwaa muhimu pia kwa wachezaji wapya wa klabu hiyo kupewa nafasi ya kuonesha uwezo wao na kuanza kuielewa falsafa ya Yanga.
“Sio jambo rahisi mara moja, linahitaji kuchukuliwa hatua kwa hatua. Kupitia mashindano haya naamini wachezaji wetu wapya watapata nafasi ya kujifunza na kutuonyesha kile walichonacho,” amesema Pedro.
The post YANGA YAANZA KOMBE LA MAPINDUZI KWA KUJIAMINI appeared first on Soka La Bongo.





