BAADA ya kuaga mashindano ya Kombe la Mapinduzi kufuatia kipigo kutokazam FC, Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amesema kutokuwepo kwa nyota wake muhimu kumeigharimu timu hiyo kushindwa kupata matokeo yaliyotarajiwa.
Barker amesema Simba iliingia kwenye mashindano hayo ikiwa haijakamilika kikosi chake kikuu, hali iliyosababisha ugumu mkubwa katika kupanga mbinu na kuhimili ushindani, hasa katika hatua za mtoano.
Ameongeza kuwa baadhi ya wachezaji muhimu walichelewa kujiunga na kambi ya timu kutokana na majukumu mengine, akiwataja Jean Charles Ahoua, Elie Mpanzu, Jonathan Sowah pamoja na mshambuliaji Steven Mukwala.
Kocha huyo amesema licha ya changamoto hizo, Simba ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini ikashindwa kuzitumia ipasavyo, jambo lililoigharimu timu ushindi na hatimaye kuondolewa kwenye mashindano hayo.
“Tumebaini mapungufu yetu, hususan katika umaliziaji wa nafasi, na tayari tumeyaweka mezani kuyafanyia kazi kabla ya mechi zijazo,” alisema Barker, amesisitiza maandalizi yameanza kuelekea michezo ya kimataifa.
Akizungumzia mchezo ujao wa kimataifa dhidi ya Esperance Sportive de Tunis, Barker alisema Simba haina budi kupata matokeo mazuri ili kufufua matumaini ya kusonga mbele, akisisitiza mechi hiyo ni ya heshima na hatima ya msimu wao wa kimataifa.
The post SIMBA MACHO MOJA KWA MOJA ESPERANCE appeared first on Soka La Bongo.






