DAR ES SALAAM:MREMBO wa Bongo Movie anayefanya vizuri kupitia tamthilia maarufu ya Kombolela, Chanuo Nchakali, ‘Mwamini’ amefunguka kuhusu maisha magumu aliyopitia alipokuwa darasa la saba, akisema kuwa hakuwa na rafiki wa kike wala wa kiume kutokana na hali duni ya maisha iliyomsababisha kushindwa kuoga na kupiga mswaki.
Akizungumza kwa hisia, Chanuo amesema kuwa kipindi hicho kilikuwa kigumu sana kwake kiasi cha kutengwa na wanafunzi wenzake shuleni kutokana na harufu mbaya ya mwili na mdomo.
“Mimi naona nilikuwa na bahati mbaya sana, kwa sababu nilikuwa na hali mbaya sana nikiwa shule ya msingi. Nimesomea Same. Kila asubuhi nilikuwa naamka nakamua ng’ombe, nikimaliza ndiyo naenda shule,” amesema Chanuo.
Ameongeza kuwa majukumu hayo ya asubuhi yalimsababishia kushindwa kujitunza ipasavyo kabla ya kwenda shule.
“Kwa hiyo nilikuwa siogi, sipigi mswaki. Nikifika darasani harufu inabadilika, ndiyo maana sikuwa na rafiki wa kiume wala wa kike,” amesema.
Licha ya changamoto hizo, leo Chanuo Nchakali ni miongoni mwa waigizaji wanaofanya vizuri kwenye tasnia ya filamu na tamthilia nchini, hali inayoonesha kuwa hali uliyonayo leo haifafanui hatma yako ya kesho.
The post Chanuo afunguka maisha magumu ya utotoni first appeared on SpotiLEO.





