UONGOZI wa Klabu ya Simba umejitokeza hadharani na kutoa tahadhari kali kwa wanachama, wadhamini na mashabiki wake dhidi ya watu wanaotumia jina na nembo ya klabu hiyo kuandaa mikutano isiyo rasmi kwa maslahi binafsi.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa leo Februari 5, 2026, Simba imeeleza kuwa imepata taarifa kuhusu watu wanaojipenyeza na kuwaita wanachama pamoja na wadhamini kwenye mikutano ambayo haijapewa baraka wala kuidhinishwa na uongozi wa klabu.
Uongozi wa Simba umeweka wazi kuwa kwa sasa hakuna mkutano wowote rasmi unaoandaliwa au kuridhiwa na klabu hiyo, hivyo umeitaka jamii ya Wanasimba kuwa makini ili kuepuka kupotoshwa au kuingizwa kwenye agenda zisizo halali.
Bodi ya Wakurugenzi ya Simba pia imeeleza kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya watu kuitisha mikutano na kutoa maneno ya kashfa pamoja na kauli zisizo na staha dhidi ya Mwekezaji wa Klabu, Mohammed Dewji.
Katika taarifa hiyo, uongozi umesisitiza kuwa vitendo hivyo visivyo vya kiungwana havikubaliki kabisa, huku ukitoa pole kwa Mohammed Dewji kutokana na kauli hizo zisizo na heshima zilizotolewa dhidi yake.
Aidha, klabu imeeleza kuwa tayari imeliandikia Jeshi la Polisi ili kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote waliohusika katika mkutano huo au waliokula njama, na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola kwa makosa ya jinai.
Bodi ya Wakurugenzi imesisitiza kuwa haitabariki wala kuvumilia mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuchafua taswira ya Klabu ya Simba, huku ikikumbusha kuwa mikutano yote halali ya klabu hutangazwa kupitia njia rasmi za mawasiliano ikiwemo tovuti, mitandao ya kijamii ya klabu na taarifa kutoka kwa viongozi waliothibitishwa.
Katika kuonesha msimamo mkali, Simba imetangaza kuwa itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu au kikundi chochote kitakachobainika kutumia nembo au jina la klabu bila ruhusa rasmi ya uongozi.
Klabu imewataka wanachama, wadhamini na mashabiki wake kuendelea kuiunga mkono Simba kwa kufuata taratibu sahihi, na kutoa taarifa mara moja pale wanapokutana na shughuli zozote zenye utata.
Hata hivyo, baadhi ya wanachama na mashabiki wameunganisha matukio hayo na kisomo cha Albadili kilichofanyika hivi karibuni, wakidai kinahusiana na kuwafichua wale wanaodaiwa kuichafua klabu.
Kisomo hicho kilifanyika Magomeni katika tawi la Mpira Pesa, ambapo baadhi ya wanachama wanaamini kimedhihirisha wazi watu wanaohusishwa na vitendo vinavyoleta mgawanyiko ndani ya klabu.
The post ALBADILI YAFICHUA MCHEZO MCHAFU SIMBA appeared first on Soka La Bongo.





