Na John Walter -Manyara
Serikali imeendelea na mkakati wa kutoa huduma za matibabu ya dharura kwa wagonjwa wanapofika kwenye vituo au hospitali kupata huduma.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa Waratibu wa afya ngazi ya mkoa RHMT pamoja na sekta ya mifugo na maji Dkt Agnes Buchwa kwa niaba ya mkurugenzi wa Huduma za dharura na maafa Novemba 10,2024 katika mji mdogo wa Mirerani wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, amesema Serikali kwa kushirikiana na Shirika la afya duniani WHO wameamua kuja na mpango huo ili kulinda afya na maisha ya Wananchi.
Dkt Buchwa ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa namna ya uendeshaji wa kituo cha kuratibu matukio ya dharura ya afya ya jamii PHEOC ambacho kinaanzishwa kwa msaada wa shirika la afya duniani WHO kwa kuwezesha vifaa vya ofisi (thamani) pamoja na ICT ambapo kwa sasa kituo hicho kipo kwenye hatua ya ukamilishwaji.
Amesema mkoa wa Manyara kama ilivyo mikoa mingine imekuwa ikikabiliana na matukio mengi ya dharura yanayoleta madhara kwa afya za binadamu, wanyama na mazingira akitolea mfano tukio la maporomoko ya tope mawe na miti mlima Hanang’ Desemba 3 mwaka,
“Kituo hiki ni moja ya mikakati ya nchi kuijengea uwezo mikoa yote 26 Tanzania bara katika kukabiliana na matukio ya dharura ya Afya ya jamii zinazoweza kujitokeza ambapo hadi sasa mikoa 16 imewezeshwa kuanzisha na kuendesha vituo hivyo (EOC) na Manyara unakuwa mkoa wa 17” amesema Dkt. Buchwa.
Mafunzo hayo ya siku tano yanatolewa na wataalamu kutoka katika kituo cha kuratibu dharura za kiafya na majanga (ECO) cha Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Ulimwenguni ofisi ya Tanzania ambayo yatawawezesha kukiendesha kituo hicho kwa ufanisi.