MAMLAKA
ya Masoko ya Mitaji na Dhamana imetoa pongezi kwa Bodi, Menejimenti na
Wafanyakazi wa benki ya CRDB kwa kutupatia furaha kubwa katika sekta ya
masoko ya mitaji, kwa kuwa mauzo ya hatifungani ya Miundombinu ya Samia
yamepata mafanikio ya asilimia 215.4, ambapo kiasi cha Sh.bilioni 323.09
kimepatikana ikilinganishwa na Sh.bilioni 150 zilizopangwa kupatikana.
Aidha,
asilimia 63.64 ya mauzo ya hatifungani imetoka kwa wawekezaji mmoja
mmoja yaani na asilimia 36.36 imetoka kwa Kampuni na Taasisi.Kati ya
wawekezaji wote walioshiriki, asilimia 99.9 ni wawekezaji wa ndani yaani
na asilimia 0.1 ni wawekezaji wa kigeni.
Hayo
yameelezwa leo Februari 18,2025 jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji
Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA)CPA. Nicodemus Mkama
wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya miundombinu ya Samia
katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.
Aidha amesema kuorodheshwa
kwa Hatifungani ya Miundombinu ya Samia, kunaongeza thamani ya
uwekezaji katika Hatifungani za Kampuni na Taasisi kwa asilimia 38.59na
kufikia Sh.trilioni 1.16, kutoka Sh.bilioni 837.31.
“Mafanikio
haya yana maana kubwa katika ustawi na maendeleo ya sekta ya fedha.
Kwanza, inaonesha imani waliyonayo wawekezaji kwa benki ya CRDB na
masoko ya mitaji. Pia masoko ya mitaji hapa nchini yamekuwa kivutio na
kutoa fursa za uwekezaji kwa wawekezaji mmoja mmoja; Taasisi; wawekezaji
wa ndani; na wawekezaji wa kimataifa.
“Tatu, kutokana na
mazingira wezeshi katika masoko ya mitaji, bidhaa mpya na bunifu
zinatolewa, hivyo kuwezesha Kampuni, Taasisi na benki kama CRDB kupata
fedha za kuendeleza na kukuza biashara; na kugharamia shughuli za
maendeleo, ikiwa ni pamoja na miundombinu ya barabara zilizo chini ya
TARURA zinazosimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
“Hivyo, tuna
kila sababu za kuipongeza Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wa benki ya
CRDB; TARURA; pamoja na taasisi na wataalamu katika masoko ya mitaji
waliowezesha kukidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Uuzaji wa
Hatifungani hii kwa umma.”
Ameongeza mafanikio hayo ni
uthibitisho wa mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kiutendaji
yanayotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi madhubuti wa
Rais Dkt. Samia Saluhu Hassan huku akifafanua lengo kuu la Hatifungani
hiyo ni kuwawezesha wakandarasi wa ndani ambao wanafanya kazi na Wakala
wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) kuwa na uwezo wa
kifedha ili kutekeleza kwa ufanisi na kwa wakati miradi ya ujenzi wa
miundombinu ya barabara vijijini na mijini hapa nchini.
CPA Mkama
amesema utoaji wa hatifungani hiyo ni hatua muhimu katika utekelezaji
wa Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha 2020/21 – 2029/30 wenye
lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi.
Pia
amesema utoaji wa hatifungani hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya
Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwani fedha zilizopatikana
zitatumika kuwezesha kampuni za kandarasi zinazomilikiwa na watanzania
kutekeleza miradi ya miundombinu kwa wakati na kwa ufanisi; na wananchi
waliowekeza katika hatifungani hiyo watalipwa riba, hivyo kuinua vipato
vyao.
“Tunaipongeza
Ofisi ya Rais TAMISEMI ambao umewezesha CRDB kushirikiana na TARURA
kutoa Hatifungani hii, hivyo kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuinua
vipato vyao; na kuwezesha kampuni za kandarasi zinazomilikiwa na
watanzania kutekeleza miradi ya miundombinu kwa wakati na kwa ufanisi.
“Kuorodheshwa
kwa Hatifungani ya Miundombinu ya Samia kwenye soko la hisa la Dar es
Salaam, pamoja na mambo mengine, kunawapatia fursa wawekezaji kuuza
hatifungani zao pale watakapohitaji fedha kwa ajili ya matumizi
mengine.”
Aidha amesema uorodheshwaji wa hatifungani katika Soko
la Hisa unawawezesha wawekezaji kujua thamani halisi ya hatifungani zao
na kuwapatia fursa wawekezaji wapya kununua hatifungani hizo, ambapo
wawekazaji hao watapata riba kama faida itokanayo na uwekezaji huo.
Ameongeza
uorodheshwaji wa hatifungani katika soko la hisa unaongeza Utawala Bora
na ufanisi katika uendeshaji wa Kampuni na kumwongezea mwekezaji wigo
na fursa zaidi za uwekezaji.Hiyo inamsaidia mwekezaji kuwa na anuwai,
jambo ambalo hupunguza athari za uwekezaji.
Pamoja na hayo CPA
Mkama amesema CRDB ni miongoni mwa kampuni ambazo zinatumia vizuri fursa
katika masoko ya mitaji na kuongeza benki hiyo imeuza hisa kwa umma na
imeorodheshwa katika soko la hisa.
Pia benki hiyo imepata
rasilimali fedha za zaidi ya Sh.bilioni 500 zilizotokana na mauzo ya
bidhaa mbalimbali katika masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na
Hatifungani ya Kijani na Hatifungani ya Miundombinu.CRDB ina leseni nne
kutoka CMSA za kutoa huduma katika masoko ya mitaji.
Amesema
kutokana na mafanikio hayo Benki ya CRDB inatekeleza mikakati ambayo
inaleta mageuzi na mafanikio yenye tija katika utendaji wa benki,
wanahisana masoko ya mitaji. Mathalani, Bei ya hisa za Benki ya CRDB
imeongezeka kwa asilimia 366.7 kutoka Sh. 150 kwa hisa wakati wa mauzo
ya hisa katika soko la awali, hadi Sh.700 kwa hisa, kwa Februari 17,
2025.
Amefafanua kama Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana
(CMSA) ilitoa idhini kwa benki ya CRDB kufanya mauzo ya Hatifungani ya
Miundombinu ya Samia yenye thamani ya Sh.bilioni 150, kuanzia Novemba
29, 2024 hadi Januari 17,2025. Idhini hiyo ilitolewa na CMSA baada ya
Benki ya CRDB kukidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Masoko ya
Mitaji na Dhamana inayohusu utoaji wa Hatifungani kwa umma.
Aidha
ametoa mwito kwa Benki zingine za Biashara, Taasisi za Fedha, kampuni
binafsi, Taasisi na Mashirika ya Umma kutumia fursa zilizopo katika
masoko ya mitaji kama ambavyo Benki ya CRDB na TARURA wametumia fursa ya
kupata shilingi bilioni 323.09 kupitia masoko ya mitaji kwa kuuza
hatifungani.