Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa (wa kwanza kushoto) akizungumza na Mwananchi Bi. Adela Bulusha (amekaa) aliyefika leo Februari 26, 2025 Katika Kambi Maalum ya uchunguzi wa awali ya afya, Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu, Kampasi ya Mloganzila kwa ajili kupima afya.
Mtaalam wa Maabara MUHAS Joseph A. Temba (kulia) akimpima Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa katika uzinduzi wa Kambi Maalum ya uchunguzi wa awali ya afya, uliofanyika leo Februari 26, 2025 Kampasi ya Mloganzila.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa akizungumza na Wananchi leo Februari 26, 2025 wakati akifungua Kambi Maalum ya Uchunguzi wa awali wa afya kwa wananchi uliofanyika Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa amefungua Kambi Maalum ya Uchunguzi wa awali wa afya kwa wananchi ambayo imelenga kutoa huduma ya vipimo vya afya bure kwa magonjwa mbalimbali itayofanyika kwa siku mbili kuanzia leo Februari 26 -27, 2025 katika Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu, Kampasi ya Mloganzila.
Kambi ni sehemu ya kumuenzi Mkuu wa Kwanza wa Chuo hicho na Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi pamoja na maandalizi ya kuelekea kilele cha kongamano litakalofanyika Februari 28, 2025 Kampasi ya Mloganzila, huku mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Akizungumza na Wananch leo Februari 26, 2025 katika Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu MUHAS Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema kuwa kwa sasa kuna magonjwa mengi yameongezeka katika jamii ambayo sio ya kuambukizwa ikiwemo moyo, mgongo, shingo ya kizazi, saratani ya tezi dume, kisukari pamoja na presha.
Profesa Kamuhabwa, amesema kuwa asilimia kubwa ya magonjwa sio ya kuambukizwa yakigundulika mapema yanatibika pamoja na kuyazuia kupitia mwenendo wa maisha kwa kutumia chakula, vinywaji pamoja na kufanya mazoezi.
“Kambi hii itakuwa endelevu na muhimu kwa wananchi kwa ajili ya kupata huduma ya vipimo pamoja na ushauri wa kiafya ambao utawasaidia kuepuka magonjwa mbalimbali, hivyo tunaomba muwe mabalozi wazuri” Profesa Kamuhabwa.
Profesa Kamuhabwa amesema kuwa upimaji wa magonjwa kwa wananchi ni sehemu ya majukumu ya MUHAS.
Ameeleza kuwa miongoni mwa majukumu yao ni pamoja na kufundisha, kufanya utafiti, kutoa huduma kwa wananchi kupitia wataalam wa aina mbalimbali katika sekta ya afya.
“Zoezi la upimaji wa magonjwa mbalimbali kwa wananchi tulianza mwaka wa jana Mkoani Kigoma, kwa sasa tuna kampasi tatu ikiwemo Muhimbili, Mloganzila na nyengine ipo Kigoma ujenzi unaendelea, lengo ni kuangalia jamii inaitaji nini kutoka kwetu kwa kufanya utafiti pamoja na kushirikiana na Wizara ya afya katika kutatu changamoto” amesema Profesa Kamuhabwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kambi Maalumu ya Uchunguzi wa awali wa afya, Dkt. Ferdinand Machiby, amesema kuwa mwitikio umekuwa mkubwa kwa wananchi kuja kupata huduma ya upimaji wa magonjwa mbalimbali, huku akieleza kuwa wanatarajia kwa muda wa siku mbili kutoa huduma kwa wananchi 600.
Dkt. Machiby amesema kuwa wamejipanga kikamilifu kutoa huduma bora ya vipimo kwa wananchi na kuwapatia matokeo pamoja na kuwashauri sehemu sahihi ya kupata huduma kwa wale watakaobainika wana matatizo ya kiafya.
“Kambi yetu ina wataalamu waliobobea katika yanja mbalimbali za afya, ambapo watatoa elimu ya afya hasa ya kujikinga na magonjwa mbalimbali pamoja na kuwashauri namna bora ya kutatua changamoto zao endapo watakuwa na matatizo yoyote ya kiafya” amesema Dkt. Machiby.
Wakizungumzia kambi hiyo, wananchi wameeleza kuwa huduma hii imekuwa mkombozi kwa familia nyingi, hasa kwa wale waliokuwa na changamoto za kifedha. “Kwa kweli, huduma hii ni ya kipekee. Tungeweza kuwa tumeathirika zaidi kiafya kama isingekuwa kwa huduma hii bure,” amesema Aisha Juma.
Pia, baadhi ya wagonjwa wameipongeza MUHAS kwa kutoa huduma bora zinazotolewa na madaktari pamoja na wa hudumu wa afya, huku wakisema huduma hizo zimeweza kupatikana kwa haraka .