Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika Machi 06 katika Viwanja vya Maonesho Dimani – Nyamazi.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika Machi 06 katika Viwanja vya Maonesho Dimani – Nyamazi.
NA Imani Mtumwa Maelezo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmin katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika Machi 06 katika Viwanja vya Maonesho Dimani – Nyamazi.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu maadhimisho hayo katika Ukumbi wa Wizara hiyo Kinazini Wilaya ya Mjini Unguja amesema Dunia huadhimisha siku hiyo kila mwaka kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa maazimio ya Kimataifa, Kitaifa na kikanda.
Amesema Zanzibar ni sehemu ya Dunia hivyo wataungana na Wanawake Ulimwenguni kuadhimisha siku hiyo kwani ni fursa adhimu ya wanawake kutoka Mikoa mbalimbali kuungana, kubadilishana uzoefu, na kujadili mbinu za kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika nyanja mbali mbali za kiuchumi.
Aidha Mhe. Pembe amesema Wizara imejipanga kuzingatia mambo muhimu katika kuadhimisha siku hiyo ni lazima kuendelea kutathmini juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali na wadau katika kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Hata hivyo ameongezea kusema kwamba maadhimisho hayo yatakwenda kuhamasisha wadau na jamii kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na kupanga mikakati mipya ya kupambana na vitendo hivyo.
Aidha ameeleza kuwa katika kuelekea madhimisho hayo huduma mbalimbali zitatolewa, ikiwemo utoaji wa mafunzo kwa wajasiriamali, maonesho ya wajasiriamali yatafanyika viwanja vya Kisonge, vipindi mbalimbali vya Redio na TV, Uzinduzi wa Muongozo wa uanzishwaji wa majukwaa pamoja na uzinduzi wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi na Mafunzo ya kuhamasisha masuala ya kupinga vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia.
Madhimsho ya siku ya Wanawake duniani kwa mwaka huu yameambatana na kauli mbiu “Ushiriki wa Mwanamke na Msichana ni kichocheo cha Maendeleo”