Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika usimamizi wa Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia Tanzania(TEITI) Bi. Mariam Mgaya,akitoa taarifa kuelekea Mkutano wa 62 wa Bodi ya Kimataifa ya TEITI utaotarajiwa kufanyika Machi 13 hadi 14 jijini Arusha.
Na.Mwandishi Wetu _Dodoma.
Ikiwa zimebaki siku kadhaa kuelekea kufanyika kwa Mkutano wa 62 wa Bodi ya EITI, Jijini Arusha, leo Machi, 10,2025 Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika usimamizi wa Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia Tanzania(TEITI) Bi. Mariam Mgaya ametoa taarifa kwa umma juu ya mkutano wa Bodi ya EITI nchini utakaofanyika tarehe 13 – 14 Machi, 2025.
“Mtakumbuka Mwezi Aprili, 2024, Tanzania ilipokea ugeni kutoka ujumbe wa Bodi ya EITI. Ujumbe huo uliongozwa na Mwenyekiti ya Bodi ya EITI, Mhe. Helen Clark ambaye alikuwa ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Newzealand na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mipango ya Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP). Ujumbe huo ulifanya kikao na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania- Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo ilikubalika Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 62 wa Bodi ya Kimatifa ya EITI” amesema Bi. Mariam.
Ameendelea kwa kusema, “Mkutano wa 62 wa Bodi ya EITI utafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 14 Machi, 2025 katika hoteli ya Gran Melia, Jijini Arusha. Mkutano huo utahudhuriwa na washiriki zaidi ya mia moja ikiwa ni wajumbe wa Bodi ya EITI kutoka mataifa mbalimbali duniani ikijumuisha wawakilishi wa kampuni kubwa zinazojihusisha na shughuli za uchimbaji na utafutaji wa rasilimali madini, mafuta na gesi asilia, Asasi za Kiraia zinazojihusisha na shughuli za uziduaji, Sekretarieti ya EITI na wawakilishi wa nchi wanachama wa EITI duniani”
Kwa upande mwingine, Bi Mariam Mgaya amesisitiza kuwa, kufanyika kwa mkutano huu hapa nchini ni fursa adhimu ya kuonesha jinsi gani nchi yetu inavyotekeleza vigezo vya kimatifa vya uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali madini, mafuta na gesi asilia kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni moja ya nchi wanachama wa EITI inayotekeleza masuala ya uwazi na uwajibikaji kisheria kupitia Sheria inayosimamia uwazi na uwajibikaji ( Sheria ya uwazi na uwajibikaji katika katika rasilimali madini, mafuta na gesi asilia Tanzania, 2015, SURA 447). Aidha, Ujio wa Bodi hiyo pia ni matokeo mazuri ya tathmini ya EITI uliofanyika mwaka 2023 ambapo Bodi hiyo ilipongeza juhudi za Serikali ya Tanzania na wadau mbalimbali katika kufanikisha utekelezaji wa shughuli za EITI hapa nchini. Matokeo ya tathmini hiyo yanaonesha kuwa Tanzania imepata alama 77/100 katika kutekeleza vigezo vya EITI vya mwaka 2019 kwa kuzingatia maeneo matatu Stakeholder engagement (82.5), Transparency(73.5) na Outcome and impact (75.5).
Mkutano huo wa Bodi ya EITI utafunguliwa rasmi tarehe 13 Machi, 2025 na Mhe. Doto Mashaka Biteko- Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Baada ya Ufunguzi wa Bodi hiyo, kutafanyika dhifa ya mapokezo ya ugeni huo na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Anthony Peter Mavunde, Waziri wa Madini. Hata hivyo, Mkutano huo utatanguliwa na Mikutano ya Kamati Ndogo za Bodi hiyo kuanzia tarehe 12 Machi, 2025.
Mkutano huo wa Bodi ni fursa kwa nchi na Watanzania kwa ujumla kwa kuwa Tanzania itapokea ugeni wa zaidi ya washiriki mia moja ikijumuisha wawakilishi wa Makapuni Makubwa duniani yanayojihusisha na Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia hivyo ni Kivutio cha Uwekezaji katika nchi yetu, Vilevile, ni fursa kuongeza fedha za kigeni kwa kuwa wageni hao watatumia bidhaa na huduma hapa nchini. Alisema Bi. Mariam Mgaya.