Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania, Division ya Ardhi.
………….
MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Ardhi imefanikiwa kutatua mgogoro wa zaidi ya miaka 20 uliohusisha umiliki wa nyumba, ambayo aliyekuwa Mtaalamu wa Shirika la Maendeleo la Taifa, Regina Ishemwabura, aliinunua kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mwaka 1973.
Jaji Elinaza Luvanda alitoa uamuzi huo hivi karibuni dhidi ya Nasor Hamis, John Mwanga na Fisha Mashoo,walalamikiwa, baada ya kumtangaza Bi Regina, mlalamikaji, kuwa ndiye mmiliki halali wa nyumba hiyo ya makazi iliyopo Kiwanja namba 705 Block ‘F’ iliyotambulika awali kuwa ni nyumba iliyopo Kiwanja namba 94A Drive Inn Cinema, Msasani.
Tayari Mahakama imemwamuru Dalali, Joshua Mwaituka, anayefanya shughuli hizo kupitia Fosters Companies Limited, kuwafukuza wadaiwa hao na kuwaondoka mara moja katika nyumba hiyo, iliyopo kando ya Barabara ya Bagamoyo.
Aidha, Mahakama imemuagiza Dalali wa Mahakama huyo kuondoa mabadiliko yote yaliyofanywa na wadaiwa bila kuathiri nyumba na kuwafukuza kwa kuvunja nyumba tajwa ili kumwezesha mmiliki halali, Bi Regina kuingia.
‘Unaamuru pia kurudisha hati hii siku au kabla ya tarehe 10 Aprili, 2025, ikionyesha namna amri hii imetekelezwa au kushindwa kutekelezwa,’ inasomeka sehemu ya amri hiyo iliyosainiwa Machi 10, 2025 na Naibu Msajili, Mhe. Mwajuma Lukindo.
Katika hukumu yake, Jaji Luvanda alipitia ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa Mlalamikaji na kujiridhisha kuwa Bi. Regina ndiye mmiliki halali wa nyumba hiyo iliyopo Kiwanja namba 705 kitalu ‘F’ ambayo awali ilitambulika kuwa ni nyumba iliyopo Kiwanja namba 94A Drive Inn Cinema Msasani kando ya Barabara ya Old Bagamoyo.
Miongoni mwa ushahidi uliotolewa ni pamoja na ule wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, kumthibitisha mlalamikaji kuwa ni mmiliki halali wa nyumba hiyo na ushahidi wa Benki ya Rasilimali Tanzania, ambapo alipata mkopo wa kununua nyumba na ripoti ya uchunguzi wa polisi juu ya madai ya kughushi, ambayo pia ilionesha kuwa hakuwa na hatia.
‘Kwa maoni yangu, kesi ya Mlalamishi iliwasilishwa vizuri na ushahidi uliotolewa ulithibitisha kuwa ana hati miliki nzuri juu ya mali hiyo. Kwa ushahidi mwingi na ripoti hiyo, haishangazi ilikuwa ndiyo sababu ya Nasor Hamis alikwepa kujitetea,’ Jaji Luvanda alisema.
Wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo, John Mwanga na Fisha Mashoo hawakufika mahakamani wala kuwasilisha hati ya utetezi kwa maandishi, hivyo shauri hilo liliendelea bila pande zote mbili kusikilizwa.
Vile vile, maelezo ya maandishi ya utetezi ya Nasor Hamis yalikataliwa baada ya kukaidi kuwasilisha maelezo ya mashahidi kama ilivyoamriwa Machi 5, 2024 na kukataa kuhudhuria tarehe na wakati ambao walipaswa kujitetea.
Mlalamikaji anadaiwa kununua nyumba hiyo kutoka kwa Shirika la Nyumba la Taifa chini ya mpango wa ununuzi wa upangaji uliendeshwa na Benki ya Nyumba Tanzania (THB).
Ilidaiwa na Mdai kuwa baada ya kununua, alikaa katika nyumba kuanzia 1973 hadi 1976 alipohamia Nairobi kuungana na mumewe, na kuacha nyumba chini ya ulinzi wa rafiki yake, Pucharis Kashaija.
Baadaye Kashaija aliihama nyumba hiyo baada ya watu fulani wanaodaiwa kuinunua. Ilikuwa ni ushahidi wa Mdai kuwa aliporudi kwenye nyumba hiyo alimkuta Karibu Ismael anayedaiwa kuingizwa humo na mjomba wake, Nasor Hamis.
Mlalamikaji anadaiwa kumfukuza Karibu Ismael kupitia amri iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. Alidai kuwa nyumba ilikabidhiwa kwake mnamo 1997 ambapo aliipangisha kwa mtu mwingine.
Kwa mujibu wa mlalamikaji, mwaka 2006 aliporudi alimkuta mpangaji wake ameondoka na John Mwanga alivamia nyumba hiyo. Alidai kuwa mwaka 2007 alipokuwa anachakata hati iligundulika kuwa mali hiyo namba 94A ilipimwa upya na kupewa jina jipya la Plot No. 705 Block A.
Mlalamikaji alidai kuwa shauri hilo lilichunguzwa polisi na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, ambapo ilibainika kuwa hatimiliki ya Nasor Hamis ilitoka kwa Fisha Mashoo aliyemuuzia John Mwanga, ambaye ndani ya mwezi mmoja aliiuza kwa Nasor Hamis.