Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii jijini Arusha leo

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii jijini Arusha leo





……………..
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Jijini Arusha leo Ijumaa Machi 14, 2025, akiwaomba Wabunge wanaounda kamati hiyo kuunga mkono Ajenda mbalimbali za maendeleo zinazowasilishwa bungeni kwaajili ya kutaka kutekelezwa na serikali mkoani Arusha.
Katika mazungumzo yao Mhe. Makonda amezungumzia miongoni mwa ajenda tarajiwa zinazohusu Mkoa wa Arusha ni pamoja na Mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kujenga reli ya kisasa (SGR) itakayotoka Mkoani Tanga kwenda mkoani Arusha kuungana na mpango mwingine wa serikali wa ujenzi wa bandari kavu mkoani Arusha itakayounganishwa na Bandari ya Tanga kwaajili ya kuhudumia nchi za DR Congo, Burundi, Uganda na Rwanda.
Kulingana na Mhe. Makonda, Bandari ya Tanga kwasasa ni ya pili kwa kupokea shehena nyingi zaidi za mizigo nchini, ikitokana na uwekezaji wa takribani Bilioni 500 zilizowekezwa na serikali, suala ambalo limesababisha barabara za Arusha kuwa na msururu mrefu wa malori kutoka 60 ya awali hadi kufikia malori 600 kwa siku yanayoelekea nchi za nje na hivyo kujengwa kwa reli hiyo ya kisasa kunatajwa kuwa kutarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji wa shehena za mizigo.
Mhe. Makonda pia ameishukuru serikali ya Rais Samia kwa kuridhia kuanza kwa uvunaji wa madini ya magadisoda kwenye eneo la Engaruka Monduli, ikikadiriwa kuvutia uwekezaji wa takribani Dola bilioni 1.5 za Kimarekani ambapo tayari serikali imetoa bilioni 14 kwaajili ya fidia kwa wananchi watakaothirika na utekelezaji wa mradi huo, akiahidi kuwa atasimamia kikamilifu utekeleza wa miradi hiyo katika kuhakikisha inakuwa na tija iliyokusudiwa kwa wananchi na serikali.