Na Ashrack Miraji Fullshagwe Media
Morogoro – Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, ametangaza rasmi nia yake ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao. Doyo alifanya tangazo hilo mbele ya waandishi wa habari jana mkoani Morogoro, na kusema kuwa kwa heshima kubwa anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjalia kuwa na afya njema.
Akizungumza kwa hisia, Doyo aliwashukuru Watanzania kwa mwitikio wao wa kuendelea kukuza demokrasia nchini, akisisitiza kuwa ni muhimu kwa kila Mtanzania mwenye sifa kupata haki ya kuchagua au kuchaguliwa. “Tanzania ni nchi ya kidemokrasia, ambapo kila Mtanzania mwenye sifa anayo haki ya kuchagua na kuchaguliwa,” alisema.
Doyo aliongeza kuwa, yeye mwenyewe ana sifa zote zinazohitajika kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akisisitiza kuwa amevuka umri wa miaka 45, umri wa kikatiba wa kugombea urais, na kwamba ana afya ya kuhimili majukumu makubwa ya urais.
Akizungumzia umuhimu wa uchaguzi mkuu ujao, Doyo alisisitiza kuwa huu utakuwa uchaguzi wa sita tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, na kwamba ni muhimu kwa maendeleo ya taifa. “Kama Mtanzania mwenye haki ya kikatiba, nimemudu kujitathmini kifikra, kiuwezo, na kiuweledi, na kujiridhisha kuwa nina uwezo wa kumudu nafasi hii,” alisema Doyo.
Doyo alifafanua kuwa uamuzi wake wa kugombea urais haujaanza kwa mkupuo, bali ni baada ya kupata busara kutoka kwa wazee na familia yake, ambao walimshauri kuendelea mbele kwa faida ya taifa. “Si busara kuwataja hapa, lakini wanajua na wanasikia wakiwa pale walipo,” alieleza.
Doyo aligusia masuala muhimu ambayo bado hayajapata kipaumbele kikubwa katika taifa letu, na ambayo ataenda kuyashughulikia iwapo atachaguliwa kuwa Rais. Masuala hayo ni pamoja na: ajira, elimu, kilimo na ufugaji, rasilimali za maji, kupambana na ukwepaji wa kodi, na kupambana na rushwa. Aliongeza kuwa ataweka nguvu katika kuimarisha sekta ya madini, kuimarisha muungano, na kuendeleza jitihada za watoto wa kike katika elimu na teknolojia.
“Kwa hiyo, nimeona ni muhimu kutoa mchango wangu kwa taifa letu ili kuleta faraja kwa Watanzania. Hivyo, leo hapa mbele yenu, mimi Doyo Hassan Doyo, mwanachama wa Chama cha National League for Democracy (NLD), natangaza nia ya kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chetu cha NLD. Dhamira yangu ni kubeba dhana ya Uzalendo, haki, na maendeleo kwa vitendo ili tuwakomboe Watanzania,” alisisitiza Doyo.
NLD: Ukombozi wa
NLD: Mtetezi wa Umma.
NLD: Moto Moto Motooo!